BALOZI WA TANZANIA MAREKANI AMJIBU TUNDU LISSU,AKANUSHA TUHUMA DHIDI YA SERIKALI

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi jana usiku walihojiwa katika kipindi cha Straight Talk Africa kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA), huku kila mmoja akipangua hoja za mwenzake.

Masilingi amekuwa balozi wa pili kumjibu Lissu baada ya siku tano zilizopita Balozi  wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi kumjibu Lissu baada ya mbunge huyo kueleza madai mbalimbali kuhusu Serikali na jinsi alivyoshambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Deutsche Welle cha nchini humo.

Katika kipindi cha jana kilichoongozwa na mtangazaji maarufu, Shaka Ssali kilichokuwa na mada ya ‘Haki ya Uhuru wa kujieleza’, kilikuwa na wanajopo wengine ambao ni Jon Temin kutoka taasisi ya Freedom House na mwanasiasa wa upinzani wa Uganda, Robert Chagulani maarufu kama Bobi Wine.

Akijibu maswali ya mtangazaji huyo kuhusu uhuru wa kujieleza na sababu ya Lissu kushambuliwa kwa risasi, Balozi Masilingi amesema licha ya eneo aliloshambuliwa kuwa ni la nyumba za Serikali lakini halina uhusiano na kubanwa kwa uhuru wa kujieleza.


Kwa upande wake Tundu Lissu alipinga hoja inayotolewa na serikali kuwa yeye anazuia uchunguzi kufanyika baada ya shambulizi la risasi lililofanywa na watu wasiojulikana dhidi yake na dereva wake nchini Tanzania.

“Kama ningelikufa na dereva wangu angelikufa kusingekuwa na uchunguzi?” alihoji Lissu.

Akijibu shutuma zilizotolewa na Lissu, Balozi wa Tanzania, Marekani kwanza alikosoa lugha anayotumia Lissu na kusema kuwa anasikitishwa na kitendo chake cha kutotambua kwake kazi nzuri ya serikali.

“Kutotambua kazi nzuri ya serikali ukazunguka dunia nzima unamtukana rais wako, vyombo vya dola, na kuwaambia watanzania kwamba hamna haki nchini kwenu sio sawa,” alisema Balozi huyo na kungeza;

“Kitendo cha Lissu kuzunguka dunia nzima hakisaidii. BBC, Radio Ujerumani -DW, Sauti ya Amerika -VOA, sio mahakama. Unachofanya ni kutuchafua na kutuvunjia heshima na kujichafua yeye mwenyewe.”

Lissu alipoulizwa dhana hasi juu ya kutembea kwake nchi za nje akieleza hali ya taifa la Tanzania na vitendo vya mashambulizi alivyofanyiwa kuwa ni kitendo cha kulichafuwa taifa au yeye kuwa ni adui wa Tanzania, alieleza:

“Lazima tutofautishe kati ya serikali na taifa. Serikali sio taifa. Serikali inatakiwa kuongozwa na katiba, na katiba yetu imeweka wazi mipaka ya mamlaka. Sisi raia ambao ndio taifa tunahaki ya kuwakosoa viongozi wetu” alieleza Tundu Lissu

“Kwa hivyo tunapoeleza juu ya matendo mabaya iwe tuko ndani ya Tanzania, au nje ya Tanzania au mahali popote tunatimiza wajibu wetu kama raia,” alisisitiza Lissu.

Akijibu hoja hiyo ya Lissu, Balozi alisahihisha kwa kusema kuwa nafasi ya rais na amiri jeshi mkuu wa nchi, ni nembo ya taifa na hivyo (raia) hutakiwi kumtukana rais.

“Unazungumza vitu ambavyo havipo na unapaswa uniheshimu kwa sababu mimi ni kaka yako,” Alisema Balozi  na kuongeza;

“Mimi kama Balozi nimekuja hapa kutetea heshima ya Tanzania, kwa kuwa wewe umekuwa ukitukana nchi yako,”

Balozi alimkumbusha Tundu Lissu kuwa kama kuna sababu zozote za kiushahidi, Tanzania ina Katiba ,inasheria, inamahakama huru na inabunge.

Katika majibu yake Lissu alisema, “Nilishambuliwa kwenye nyumba za Serikali, nilipigwa mara 16 na nimefanyiwa operesheni 22. Swali la kujiuliza, nani aliyetoa agizo la kuondoa ulinzi katika nyumba za Serikali?”

“Pili, hilo eneo linalindwa na CCTV (kamera) ziliondolewa siku moja kabla ya tukio. Hakuna anayejua zilikopelekwa kwa sababu polisi hawasemi zilipelekwa wapi. Ninazungumza na watu, hakuna mtu aliyehojiwa.”

Hata hivyo Balozi alimjibu Tundu  Lissu akisema: "Wewe ulikuwa hospitalini mwaka na nusu unaletewa taarifa za kukuchonganisha na serikali na unazikubali kama zilivyo. Wewe kama mwanasheria huwezi ukachukua ushahidi wa kuambiwa.

"Kama mnadhamira ya dhati ya kutaka uchunguzi ufanyike, kwa nini hutaki kurudi nyumbani ukatoe ushahidi wewe na dereva wako na badala yake unazunguka kutukana na kuichafua nchi"

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post