Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimeandika barua kwenda kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino likimshtaki Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa kutoa kauli za kibaguzi na unyanyasaji.
Katika barua hiyo ya kurasa mbili, iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumain Makene imeonyesha masikitiko yake kwa kitendo cha Karia kutumia mchezo wa soka kuonyesha chuki na ubaguzi dhidi ya Tundu Lissu ambaye Septemba 7, 2017 alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma.
"Tunaandika barua hii kuelezea masikitiko yetu na kupinga kauli iliyotolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia ambayo inaunga mkono uvunjaji wa haki za binadamu, uhuru wa kuzungumza na kuchochea ubaguzi wa kisiasa jambo ambalo ni kinyume na miiko ya mchezo wa mpira wa miguu unaosimamiwa na Fifa," imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo ambayo pia imeelekezwa kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Karia mwenyewe, imeambatanishwa pia na ushahidi wa kipande cha video kinachomuonyesha Rais huyo wa TFF akitoa kauli hiyo.
February 2 2019 shirikisho la soka Tanzania TFF lilifanya mkutano mkuu wa mwaka shirikisho hilo jijini Arusha na kujadili mambo mbalimbali, moja kati ya vitu vilivyoibuka katika mkutano mkuu ni kauli ya Rais wa shirikisho hilo Wallace Karia alipotaja jina la Tundu Lissu akimtolewa mfano Michael Wambura.
Michael Wambura alikuwa Makamu wa Rais wa TFF kabla ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka, hivyo Wambura kwa sasa ni kama ana mpinga Karia kiasi cha Wallace Karia kumfananisha Wambura na Mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya CHADEMA Tundu Lissu.
Karia alinukuliwa akisema kauli inayoeleza kuwa atawashughulikia wakina Tundu Lissu wa soka akimlenga Wambura, kitu ambacho hakijawafurahisha CHADEMA na sasa wameamua kuandika barua kuipeleka shirikisho la soka Ulimwenguni FIFA kumshitaki Wallace Karia.