Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru wadhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chama cha Chadema, Tundu Lissu kufika Mahakamani hapo Februari 25, 2019 kueleza maendeleo ya afya yake.
Amri hiyo, imetolewa leo Februari 4, 2019 baada ya Wakili wa serikali Mwandamizi Patrick Mwita kudai mahakamani hapo, Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na kwamba hadi sasa hawajajua hali ya mshtakiwa wa nne, ambae ni Lisu inaendeleaje.
"Mheshimiwa, Kesi hii leo imekuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa lakini hadi sasa hatuna taarifa ya hali ya mshtakiwa wa nne,tunaamini hata Mahakama hii haina rekodi ya Maendeleo yake" amedai Wakili Mwita
Hakimu Simba amesema, kwa kuwa mahakama hiyo haina rekodi ya taarifa ya hali ya Lisu hivyo Februari 25 wadhamini wafike Mahakamani ili kueleza maendeleo ya afya yake.
Kesi hiyo ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, inamkabili Lissu na wenzake Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Kwa pamoja, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa, Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Social Plugin