Na January Makamba
Ndugu yangu Ruge, najua ndio umewasili huko upande wa pili na si ajabu una mambo mengi na bado unasalimiana na jamaa zetu wengi waliotangulia.
Lakini naomba uchukue muda wako kidogo kunisikiliza. Nimeumia sana na nimelia peke yangu kwamba umetuacha namna hii. Sawa, umeitwa kwa wakati wako na sisi hatuna kauli kwenye suala la wakati wa kuitwa lakini nilitegemea, na sikuwa na shaka kabisa, kwamba tutakamilisha yale mawazo yako mengi mazuri uliyoniambia. Sikuwa na shaka kwasababu nilishuhudia pale Hospitali ya Kairuki kabla hujaenda India, ulivyorudi kutoka India, na siku nimekuona Afrika Kusini, ulivyokuwa unapigana kupona — hadi madaktari wa Afrika Kusini wakakupa jina “Ruge, The Fighter”. Jina sahihi kabisa lililotafsiri harakati za maisha yako.
Unajua nini? Nilikuwa nangoja urudi Dar nikwambie nilichogundua mara ya mwisho nilivyokuona hospitali. Lakini ngoja tu nikwambie kabla sijaja huko uliko. Ile kiu kubwa ya kupona niliyoiona kwenye macho yako haikuwa kwa ajili yako wewe, bali kwa ajili ya kutoiangusha familia yako nzima iliyosimamisha kila kitu kukuuguza na Watanzania wote waliokuwa wanakuombea. Ulipigana kupona, sio kwa ajili yako, bali kwa ajili yetu. Hukuamka kitandani lakini hukushindwa mapambano kwasababu umeamkia ndani ya mioyo ya Watanzania. Huku tuliko karibu watu wote tunakumbuka ulivyotugusa. Jamaa yangu, tunakuomboleza wakati huu, halafu tutabaki tunafurahia nuru yako katika maisha ya wengi kwa urefu wa uhai wetu. Umekimbia mbio njema, umemaliza safari yako vyema.
Majonzi yangu ni kwamba umeondoka kabla sijalipa kwa ukamilifu deni langu kwako. Deni la upendo na urafiki wa kweli. Ulinipa heshima kubwa ya kuwa msiri wako — kwa kuniamini na kunielezea wasiwasi wako, ndoto zako, matumaini yako, harakati zako, mipango yako. Ulinipa heshima ya kunipa fursa ya kubishana nawe kuhusu mawazo na fikra zako.
Majonzi yangu ni kwamba kuna vitu fulani vikubwa na vizuri tulivipanga — mimi na marafiki na wadogo zako, kwa ajili yako, kwa staili yako — mapema mwezi Machi, ambavyo naamini vingekupa tabasamu. Kama unaweza, hapo ulipolala, tupe ishara tufanyeje.
Nafarijika kidogo kwamba nilipata nafasi ya kukukumbatia kwa mara ya mwisho. Sikujua kwamba tunaagana. Ulinishika mkono kwa nguvu, hukutaka kuuachia, na ulitabasamu niliposema nakungoja Dar tukae pale THT, kama kawaida yetu, kujadili mawazo na mipango yako mingi.
Ingawa umeshawasili huko upande wa pili, familia yako na watu wengi watauaga mwili wako kwa heshima kubwa. Utajengewa kaburi. Nadhani litawekwa marumaru. Lakini tukitaka kukusalimia tena hatutakutafuta kaburini kwako. Tutakutafuta kwenye nyoyo za watu uliowagusa na kuwasaidia. Na ni wengi kweli. Kumbukumbu yako itabaki kwenye nyoyo zao na kwenye mafanikio yao. Watoto wako hawapo peke yao. Watalia sana, lakini ni kwa muda tu; kwasababu watafunikwa kwa upendo wetu sote na watafarijika, na watakuwa na fahari, kwa jinsi unavyosemwa na unavyokumbukwa.
Ndugu yangu, nisikuchoshe. Mengine tutaongea tutakapokutana tena kwasababu kwa hakika sisi sote, mmoja mmoja na kwa wakati wetu, kwa kadri ya mipango ya yeye aliyetuumba, tutakufuata huko. Miaka yote nimekujua, sijawahi kukuona umepumzika. Pumzika kwa amani kwa sasa — na milele.
Ndimi, rafiki yako,
January Makamba
27 Februari 2019
Social Plugin