Kumetokea kisa cha ajabu mjini Matuu Kaunti ya Machakos nchini Kenya baada ya mfanyabiashara maarufu eneo hilo kukutwa katika gari lake akiwa amefariki huku ameshikilia sahani ya wali na pembeni kukiwa na chupa ya chai moto.
Wengi walioshuhudia walipatwa na mshtuko mkubwa na haijabainika iwapo aliuawa ama aliaga dunia kwa njia ya kawaida.
Mkuu wa polisi eneo la Yatta Eric Ng'etich amethibitisha tukio hilo na kusema, marehemu alikuwa amekamata sahani ya wali na pembeni kulikuwa na chupa ya chai moto.
Polisi walisema kwa sasa hawawezi kuthibitisha kilichomuua mfanyabiashara huyo lakini uchunguzi wao umeanzishwa.
"Ni masikitiko kwa visa vya aina hii. Marehemu ni Joe, mfanyabiashara maarufu hapa. Alipatikana akiwa maiti ndani ya gari lake. Hatuwezi kufahamu ikiwa ni kweli alikuwa akila wali ama sahani na chupa ya chai alilazimishiwa," Ng'etich alisema.
"Uchunguzi umeanzishwa. Tutachunguza hadi tutakapopata ukweli kuhusu kifo chake," mkuu huyo wa polisi alisema.
Alisema kuwa, walivunja mlango wa duka la marehemu lililokuwa karibu na kukuta pingu zilizokuwa juu ya kaunta.
Wakazi wa eneo hilo ambao sasa wana hofu kufuatia mauaji hayo, wanahusisha mauaji hayo na kisa cha 2018 ambapo mfanyabiashara mwingine aliuawa katika eneo hilo.
Jumatano, Novemba 14, Peter Mwangangi mfanyabiashara maarufu wa eneo la Kanyonyoo, Machakos alipataikana amekufa katika gari lake aina ya Toyota Harrier na polisi kushuku aliuawa kwa kudungwa sindano zenye sumu.
Social Plugin