Bwana mmoja raia wa Nigeria aitwaye Enango Gelsthorpe Sege ameuawa kwa kupigwa na majambazi waliojihami kwa silaha baada ya mke wake kujigamba mtandaoni /facebook akiwa na mabunda ya pesa zake.
Mtu anayedai kuwa kaka yake marehemu, kwa masikitiko makubwa alisema alipokea taarifa kuhusu kifo hicho Jumanne, Februari 5,2019.
Enango Gelsthorpe Sege aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi baada ya mke wake kujigamba mtandaoni akiwa na mabunda ya pesa.
Ibomo Rafeal Seimiengha, ambaye ni kaka ya marehemu alisema kwamba, Enango alishambuliwa na majambazi hao na hatimaye kupigwa risasi.
"Nilipata habari hizi za kutisha jana. Kaka yangu alipigwa risasi nyumbani kwake na watu wasiojulikana waliokuwa wamejihami kwa silaha. Ni makosa ya mke. Mke alichapisha picha Facebook akiwa na mabunda ya pesa. Kaka yangu alikuwa amelipwa na kampuni yake. Lala Salama Enango Gelsthorpe Sege.",alieleza.
Inaelezwa kuwa marehemu aliuawa akiwa nyumbani kwake na majambazi hao walivunja na kuingia bila ya yeye na mke wake kufahamu.
Kabla ya kifo chake, Enango alikuwa amelipwa na mwajiri wake na aliamua kwenda na mabunda ya noti nyumbani kwake.
Kisha mke wake aliyekuwa na furaha mpwitompwito alijipiga picha akiwa na mabunda ya noti hizo mkononi na kuzianika mtandaoni.
Katika picha hizo, ilikuwa bayana kwamba, mke wake Enango aliutaka ulimwengu mzima kuona jinsi walivyokuwa na utajiri wa pesa lakini mwisho ukawa mbaya sana.