Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKURUGENZI WA HALMASHAURI MBARONI TUHUMA ZA KUUA KWA RISASI KANISANI SINGIDA


Watu watano, akiwamo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida, wakituhumiwa kusababisha kifo cha mfugaji Peter Chambalo, anayedaiwa kupigwa risasi akiwa kanisani. 

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi,jana alikiri kutokea kwa tukio hilo juzi na kueleza kuwa mpaka sasa, wanaoshikiliwa ni watu wa watano akiwamo mkurugenzi huyo. 

Msangi alitaja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kuwa ni askari wanyamapori wawili, mmoja kutoka Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) na mwingine kutoka Halmashauri ya Ipigi, mwanasheria na mtendaji wa kata. 

“Ni kweli tukio limetokea, lakini siyo kweli kuwa askari wa Jeshi la Polisi wamehusika na tukio hilo," Msangi alisema, "kwanza hawakuwapo kwenye tukio hili. 

"Waliokuwapo ni askari wanyamapori, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, mwanasheria wake na mtendaji wa kata. Kilichotokea ni kwamba, walipofika katika kijiji cha Kazikazi, Kata ya Kitaraka, Tarafa ya Itigi, kulitokea kutoelewana, hivyo kusababisha vurugu," alisema. 

Aliongeza kuwa, wakati wa vurugu hizo, inadaiwa askari walifyatua risasi na kumjeruhi mtu huyo ambaye alifariki dunia. 

“Uchunguzi wa tukio hili unaendelea na hivi sasa Mkuu wa Mkoa huo, Kamanda wa Polisi wapo eneo la tukio kupata maelezo zaidi, hizi ndizo taarifa nilizonazo hadi sasa,” Msangi alisema. 


Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi alisema suala la mauaji si la kisiasa wala kiutendaji, hivyo linapaswa kujibiwa na Polisi, “Mtafuteni kamanda wa polisi Mkoa wa Singida anaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia.”

Alipotafutwa, kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida simu yake iliita bila kupokewa.

Mchungaji wa Kanisa la Adventista Sabato yalikotokea mauaji hayo, Manyigina Manyigina alisema alipata taarifa hizo akiwa Manyoni alikokuwa akiendesha ibada nyingine na alilazimika kukatisha ibada na kurejea Itigi ili kujua kilichosababisha tukio hilo.

Alisema alisimuliwa lilivyokuwa na waumini ambao walidai kabla ya mauaji hayo, kulitokea vurugu kanisani hapo wakati wa mafundisho ya sabato saa saba mchana.

“Waumini walinieleza kuwa baada ya kupata chakula cha mchana kanisani hapo, wengine walikuwa wameingia ndani na wengine walikuwa nje, ndipo waliona gari mbili aina ya Land Cruiser za Serikali zikiingia eneo hilo na mkurugenzi alishuka na maaskari watatu.

“Nje walimkuta mzee mmoja wakampiga kisha wakaingia kanisani na kumkaba shati muumini mmoja kabla ya kumkata ngwala na walikuwa wakiulizana ni huyu... hapana siyo huyu wanaulizana na kujibizana wao kwa wao, kisha ofisa mtendaji waliyeongozana (hakumtaja jina) naye akawaambia watoke nje,” alisema. Alidai kuwa walipotoka nje, waliwafungia waumini mlango kwa nje na baada ya muda walirudi na kumpiga risasi muumini mmoja ambaye alifariki dunia papo hapo.

“Najiuliza kwa nini wamekuja kufanya fujo kanisani tena siku ya sabato na kuua, inashangaza sana,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com