RPC ASIMULIA TUKIO LA MAUAJI KANISANI "DED ALIFUNGA MLANGO WA KANISA,ASKARI WAKAFYATUA RISASI"



Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert  Njewike akizungumza na waandishi wa habari leo

Kanisani baada ya tukio

Na  Sylivester Richard - Singida 
Jeshi la polisi mkoani Singida linawashikilia watu 7 kutokana na tuhuma za mauaji ya  Isaka Petro , (28), mkazi wa kijiji cha Kaskazi, Tarafa ya Itigi  Wilaya ya Manyoni ambaye  alifariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na kitu kunachodhaniwa kuwa ni risasi upande wa kisogoni wakati akiwa kwenye ibada na waumini wenzake katika kanisa la Sabato lililoko kijijini hapo.


Akiongea na waandishi wa habari leo Jumanne Februari 5,2019, Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert  Njewike amewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni pamoja na Pius Shija, (54), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi, Silvanus  Lungwsha, (50), Afisa kilimo na mifugo - Itigi na Elik Paulo , (31) Afisa Sheria Itigi. 

Wengine ni Eliutha Augustino, (43), Afisa Tarafa - Itigi , Yusuph John , (25), Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaskazi, mkazi wa Itigi, Rodey Elias ,(42) Afisa wanyamapori mwajiriwa wa Halimashauri ya Itigi na Makoye Steveni Askari wa wanyamapori Hifadhi ya Doloto.

Kamanda Njewike ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea siku ya tarehe 02.02. 2019 majira ya saa 8:20 mchana huko katika kijiji cha Kaskazi, Tarafa ya Itigi  Wilaya ya Manyoni ambapo Isaka Petro , (28), mkazi wa kijiji hicho alifariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na kitu kunachodhaniwa kuwa ni risasi upande wa kisogoni wakati akiwa kwenye ibaada na waumini wenzake katika kanisa la Sabato lililoko Kijijini hapo.

Njewike amesema Marehemu aliuawa baada ya Maafisa 7 wa Halimashauri ya Itigi wakiongozwa na Pius Shija -  Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri hiyo kuwatafuta watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali lililotokea tarehe 01.02.2019 ambapo mlalamikaji Rose Andrew alidai kuharibiwa mali yake iliyopo ndani ya shamba la Tanganyika Parkers linalomilikiwa na Halimashauri hiyo.

Hata hivyo Kamanda ameleza kuwa Maafisa hao walipata taarifa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali wapo katika kanisa la Wasabato lililopo Kijijini hapo ndipo walipokwenda kwa lengo la kuwakamata. 

Ameongeza kuwa baada ya Mkurugenzi kuingia ndani ya Kanisa hilo kulitokea vurugu ndipo Mkurugenzi huyo alienda nje  na kufunga mlango kwa nje na askari wa wanyamapori waliokuwa na silaha walifyatua risasi kadhaa ambapo mmoja alimpiga Marehemu kisogoni na kufariki dunia papo hapo .

 Kamanda amefafanua kuwa watuhumiwa bado wanashikiliwa kwa uchunguzi na muda wowote watafikishwa Mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post