Wakazi wa kijiji cha Ober, Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya wameshangazwa na tukio la mwanaume aitwaye Paul Ochieng', (21) kujiua mara baada ya kumpiga mpenzi wake Beryl Atieno na kumtoa uhai.
Inadaiwa Paul Ochieng' aligombana na mpenzi wake Beryl Atieno, 18, Ijumaa, Februari 1,2019 kabla ya kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa majirani walioshuhudia tukio hilo, ndoa ya Ochieng na binti huyo ilipingwa sana na mama mkwe aliyetaka binti yake kurejea katika boma lao ili kuendelea na masomo, Citizen Digital iliripoti Jumapili, Februari 3,2019.
Akithibitisha kisa hicho, Chifu wa eneo hilo Chief Mark Ongoro alisema marehemu hao walikuwa katika uhusiano uliokuwa umedumu karibia miezi kumi.
Ongoro alisema Atieno alikuwa amerejea katika nyumba yao kuchukua virago vyake wakati Ochieng' alipopandwa na hasira na kufanya unyama huo.
Baada ya kugundua mchumba wake alikuwa amerejea nyumbani, majirani wanasema Ochieng' alikwenda sokoni na kununua sumu na kamba na kurejea nyumbani na kuanza kumpiga mke wake hadi kumuua.
Ochieng' alikunywa sumu na kujitia kitanzi shingoni kabla ya majirani kuingilia kati na kumpeleka hospitalini alikokata roho akipokea matibabu.
Miili ya wawili hao ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Homa Bay huku polisi wakianzisha uchunguzi wao kuhusu kisa hicho.
Via Tuko
Social Plugin