Polisi huko Homa Bay nchini Kenya wamewatia mbaroni baba na mwanae wa kiume kwa kumpiga hadi kumng’oa meno afisa wa polisi aliyekuwa ameenda kumkamata mshukiwa mwingine aliyehusishwa na mzozo wa shamba katika mtaa wa Ka Peter, Homa Bay.
Kwa mujibu wa ripoti ya Taifa Leo, Februari 4,2019, Boniface Oremo (48) na mwanae Collins Oremo (22) walimvamia afisa huyo kwa mawe na kumsababishia majeraha mabaya.
Inaelezwa kuwa afisa huyo alikuwa ameandamana na wenzake wawili wakati baba na mwanawe walipoanza kuwarushia mawe ili kuwazuia kufanya kazi yao.
Kulingana na ripoti hiyo, mmoja wa maafisa hao wa polisi alipoteza baadhi meno yake baada ya jiwe lililorushwa kumpata mdomoni.
Naibu Chifu wa Kata ya Asego Tom Ondiek alisema kwamba wawili hao walikamatwa baadaye wakiwa mafichoni katika mitaa mbalimbali mjini Homa Bay.
Walikuwa wamejificha baada ya kupata taarifa kwamba polisi walikuwa wakiwasaka.
OCPD wa Homa Bay Sammy Koskey alisema kuwa, afisa wa polisi alijeruhiwa amelazwa hospitalini na anaendelea kupokea matibabu huku washukiwa hao wakisubiri kufikishwa kortini.
Kwa sasa washukiwa hao wanaendelea kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay.