MWANASIASA MKONGWE TANZANIA HAMIS MGEJA ATANGAZA KUPUMZIKA SIASA

Mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Shinyanga, Hamisi Mgeja (kulia pichani) ametangaza kupumzika siasa kwa muda na kujikita kwenye shughuli nyingine.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Kahama, Mgeja amesema kwa sasa akili yake ameielekeza zaidi katika shughuli za kilimo pamoja na michezo hasa soka la watoto wadogo ili kuwajengea hamasa na kuvutia wadau mbali mbali waweze kuwekeza katika kizazi kijacho.

“Mwalimu (Julius Nyerere) alitufundisha siasa ni kilimo, nimeamua kujikita shambani kumuenzi kwa vitendo na kuhamashisha vijana kujihusisha na kilimo kitakachowaongezea tija na kipato katika maisha yao,” alisema Mgeja aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga.

“Hapa kwetu kilimo ni uti wa mgongo na ni kazi kama nyingine. Kwa kuwa Mwalimu alisema kazi ni kipimo cha utu, nawahamasisha vijana waje shambani tuungane pamoja kujiletea maendeleo" amesema.

Hivi karibuni, Mgeja ameonekana kwenye majukwaa ya michezo hasa soka la vijana wadogo.

Kuhusu hilo Mgeja amesema, “Soka letu ili lisonge mbele upo wajibu kwa wadau kuwekeza katika soka la watoto na ndio maana tumeanzisha Kahama United Sports Academy ili kukuza vipaji vya watoto wadogo.

“Kwa kutambua mchango wangu wadau wamenipatia heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini nikishirikiana na wadau wa michezo wilayani Kahama chini ya Mwenyekiti wetu, Charles Lubala na Katibu wake, Mwalimu Daniel Mbilinyi. Ipo siku soka letu litafika pale tunapopatarajia kama wadau watainuka na kuungana pamoja nasi huku chini kwenye kuvumbua na kukuza vipaji,” amesema.

Mgeja alikuwa mmoja kati ya majina ya wanasiasa wakongwe waliosikika zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, baada ya kuihama CCM na kujiunga na Chadema kumuunga mkono swahiba wake aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyeshindwa.
CHANZO - HABARILEO

Hamis Mgeja (kulia) akimpatia jezi mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi kweny moja ya shughuli za kimichezo za Hamis hivi karibuni mjini Kahama (Picha kutoka Maktaba ya Malunde1 blog)


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post