Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa, amewataka watumishi wa umma kuwa na subira kwa sababu Serikali inaendelea na mchakato wa kuwatambua watumishi wa umma halali na kufanya ulinganifu wa mishahara katika kada mbalimbali ili watumishi hao waanze kulipwa mishahara stahiki.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyazungumza hayo leo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Mhe Pascal Haonga, lililohoji juu ya ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa mwanzoni nchi ilikuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi hewa ambapo wote kwa pamoja walikuwa wakilipwa mishahara na posho mbalimbali hivyo, ili kuwatambua watumishi halali Serikali iliamua kufanya uchunguzi na kuwagundua watumishi hao hewa.
Pia, Serikali ilifanya uchunguzi mwingine wa kuwatambua watumishi wenye vyeti stahiki vya kufanya kazi mbalimbali Serikalini kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa baada ya kumaliza utambuzi wa watumishi halali, Rais Dkt. Magufuli aliunda Tume ya Mishahara na Motisha kwa ajili ya kufanya mapitio ya kada zote za Utumishi wa Umma na viwango vya mishahara ili kutambua ulinganifu kati ya stahiki ya mshahara na kada husika.
"Lengo la Rais Magufuli kuunda tume hiyo ni kufanya tathmini nzuri ili kutambua weledi wa kazi, uwajibikaji na tija inayopatikana mahala pa kazi, hivyo baada ya kukamilika Serikali itatoa taarifa," alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe. Majaliwa ametoa rai kwa Watumishi wa Umma kuendelea kuiamini serikali kwani ina nia ya dhati kuhakikisha watumishi wote wanapata haki zao stahiki vile vile mpaka sasa mjadala kati ya Serikali na Vyama vya Wafanyakazi unaendelea vizuri.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Social Plugin