Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAKAMA YAMUACHIA JAMAA ALIYETOROSHA MTOTO KWENYE BEGI HOSPITALI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Milimani jijini Nairobi, Kenya leo imemuachia kijana aliyekamatwa akimtorosha mwanawe wa kike kutoka Hospitali ya Taifa Kenyatta (KNH) kukwepa deni la tiba alilokuwa akidaiwa.

Februari 16 mwaka huu, walinzi wa hospitali hiyo walimkamata Boniface Murage (22) akikitorosha kichanga chenye mwezi mmoja kwa kukiweka kwenye begi la bluu.

Kichanga hicho kililazwa hospitalini hapo Januari 26 mwaka huu, na kiliruhusiwa Februari 11, na hadi kinatoroshwa wazazi walikuwa wanadaiwa shilingi 56,937 za Kenya.

Murage alipandishwa kizimbani jana na alikiri kutenda kosa hilo kwa kuwa hakuwa na fedha za kulipa deni alilodaiwa.

Kijana huyo pia aliieleza Mahakama kuwa, alifanya hivyo pia kwa kuwa aliogopa endapo asingekuwa mbunifu mkewe na mwanawe wasingeruhusiwa kuondoka hospitalini hapo.

“Ni kweli. Ndiyo nilitaka kumtorosha mwanangu…niliogopa kwamba binti yangu na mke wangu wangezuiwa pale hospitalini kwa muda mrefu kwa sababu sikupata fedha Ksh 56,937 za kuilipa hospitali”alisema Murage.

Wasamaria wema walilipa deni hilo jana saa 12 jioni. Mke wa Murage na mwanawe waliruhusiwa jana kuondoka hospitalini.

Hakimu wa Mahakama ya Milimani, Caroline Nzibe amemuachia Murage kwa miezi mitatu kwa sharti kwamba katika muda huo asifanye kosa lolote.

Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa mshitakiwa, Charles Madowo, aliiomba Mahakama imuachie mteja wake kwa kuwa fedha alizokuwa akidaiwa zimeshalipwa.

Gavana wa Jiji la Nairobi, Mike Sonko amesema, amefurahi kijana huyo ameachiwa, na kwamba, jana yeye na wenzake walinunua vitu kwa ajili ya familia ya Murage.

Awali, Wakili wa Murage aliiomba Mahakama imuonee huruma kijana huyo kwa kuwa tangu aliposhitakiwa alitoa ushirikiano kwenye mchakato wa kesi.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, Februari 16 mwaka huu, Murage alitaka kumtorosha mwanawe kuukwepa utawala wa KNH.

Wakati kijana huyo akiondoka hospitalini hapo, walinzi walimlazimisha afungue begi alilokuwa amebeba na wakakuta kitoto hicho.
Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com