Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, katika kikao chake cha 196 limemsimamisha Muuguzi Martin Chama kutoa huduma za Uuguzi na Ukunga kwa muda wa mwaka mmoja tangu tarehe 7.02.2019 baada ya kumtia hatiani na makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa katika Baraza la Uuguzi na Ukunga mwezi Septemba 2018.
Makosa hayo ni pamoja na kufika kazini akiwa amelewa na kutaka kuhatarisha usalama wa wagonjwa na ndugu zao kwa kushindwa kutoa huduma kwa umakini na weledi.
Awali ofisi ya Msajili wa baraza la Uuguzi na Ukunga lilipokea tuhuma kutoka Hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mount Meru Arusha kupitia kwa Muuguzi mkuu wa mkoa ambaye pia ni msimamizi wa maadili wa mkoa wa Arusha kwa mujibu wa sheria N0 1ya mwaka 2010.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo muuguzi huyu alifika kazini tarehe 26.09.2018 zamu ya usiku majira ya saa tatu husiku akiwa amelewa na alianza kuwasumbua ndugu waliokuwa wakiwaangalia wagonjwa wao kutaka kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa ili hali akiwa amelewa sana hali ambayo ingesababisha kuhatarisha maisha ya wagonjwa kwa kuwa hakuwa na umakini.
Tuhuma hizi ziliwasilishwa na walalamikaji wawili waliokuwa wakiuguza wagonjwa wao.
Ofisi ya Msajili ilituma Afisa kutoka baraza la Uuguzi na Ukunga ambaye aliungana na timu ya Mkoani Arusha ikiongozwa na Muuguzi mkuu wa Mkoa wa Arusha.Timu hii ilifanya uchunguzi wa awali na kubaini mapungufu yaliyofanywa na muuguzi huyu ambayo ni kinyume na maadili ya Uuguzi na Ukunga.
Taarifa hiyo ilipelekwa katika kikao cha dharura cha bodi cha 195 ambacho pamoja na mambo mengine ilijadili taarifa hii na kuamua shauri hili lisikilizwe kataka kikao cha bodi cha 196 ambayo itahusisha mtuhumiwa na mashahidi ambao ni walalamikaji na watumishi waliokuwepo siku ya tukio.
Shauri hili limesikilizwa tarehe 07.02.2019 ambapo Ushahidi uliotolewa umemtia hatiani bwana Martini kwa kulewa na kushindwa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa weledi na kutaka kuhatarisha Maisha ya wagonjwa na ndugu zao.baraza liliadhimia kwa kauli moja kumsimamisha kutoa huduma hizi kwa muda wa mwaka mmoja.
Baraza la Uuguzi na Ukunga ni Mamlaka iliyoanzishwa kisheria na kufanya kazi chini ya Sheria inayoitwa The Nursing and Midwifery Act, of 2010.Baraza lilianzishwa kwa ajili ya kulinda umma kutokana na huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini na linafanya kazi kwa kusimamia ubora katika mafunzo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vilivyowekwa.
Imetolewa na
Agnes Mtawa
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga
09.02.2019
Social Plugin