Mbunge wa Mtama Nape Nnauye amewataka Wanasiasa kujiwekea utaratibu wa kuwa na akiba ya maneno pindi wanapozungumza mambo ikiwemo kupinga jambo.
Nape aliyasema hayo jana wakati akichangia mapendekezo katika taarifa mbili za Kamati ikiwemo Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa mwaka 2018 pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Alisema kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Mtama wanamshukuru Rais John Magufuli kwa kukubali maombi yao ya kufuta mashamba yaliyotelekezwa.
“Tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu. Wakati wa uchaguzi tulipeleka kwa Rais maombi ya kufuta baadhi ya mashamba yaliyotelekezwa,” alisema.
Alisema miongoni mwa mashamba hayo ambayo Rais alikubali ombi lililopelekwa kwake na yeye na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ni shamba namba 37 lililopo eneo la Maumbika jimbo la Mtama mkoani Lindi.
“Wakati mwingine tunapolishwa maneno tukaseme tuweke akiba ya maneno ya nani anapinga nini na anasema nini? Itatusaidia sana kwa sisi wanasiasa tukiweka akiba ya maneno,” alisema.
Jumatatu, Nape aliandika barua kwenda kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na hadi sasa bado haijafahamika sababu ya kujiuzulu kwake.
Social Plugin