Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakiwa kwenye Nyumba iliyojengwa mpakani mwa Tanzania na Kenya. Horohoro. Mhe. Ndumbaro akiwa upande wa Kenya na Mhe. Kijaji akiwa upande wa Tanzania.
Juma Ally, aliyejenga nyumba katikati ya mpaka Tanzania na Kenya katika kijiji cha Jasini wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga amesema haoni tatizo nyumba yake kuwa eneo hilo.
Amesema nyumba hiyo ipo katikati ya mpaka huo, na baadhi ya vyumba vyake vipo upande wa Tanzania na vingine upande wa Kenya.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 14, 2019 ikiwa ni siku moja baada ya naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kutembelea kijiji hicho.
Katika ziara yao hiyo mawaziri hao walikumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na suala la mipaka.
Katika maelezo yake, Juma amesema kuwa wao ni wakazi wa muda mrefu katika eneo hilo na hata huduma za kijamii wanazipata kutoka Kenya.
Amesema licha ya kupata huduma hizo Kenya, wao ni Watanzania.
“Nilivyojenga nilijua nimejenga Tanzania kwa kuwa ni nchi yangu ila baada ya mawaziri kufika hapa ndiyo nikasikia kuwa nyumba yangu iko upande wa Kenya na Tanzania,” amesema Juma.
Na Raisa Said, Mwananchi