Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PAPA AMVUA MADARAKA KARDINALI KWA KUBAKA MTOTO

Papa Francis amemvua madaraka kardinali wa zamani, ikiwa ni tukio la kwanza kwa Kanisa Katoliki kuchukua hatua baada ya Mmarekani huyo, Theodore McCarrick kutuhumiwa kumbaka mtoto miaka 50 iliyopita, taarifa ya Vatican imesema jana.

McCarrick, 88, ambaye alijitoa kutoka Taasisi ya Makardinali ya Vatican mwezi Julai, ni kardinali wa kwanza duniani kutengwa kutokana na tuhuma za ngono.

Mahakama ya Vatican ilimkuta na hatia ya kosa la kumbaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 20, uamuzi uliothibitishwa na Papa mwezi huu, na hivyo hauwezi kupingwa zaidi, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Ilisema McCarrick alipatikana na hatia ya “kuzini kinyume na amri ya sita kwa kufanya uzinzi na mtoto pamoja na watu wazima, na tatizo kubwa zaidi ni kutumia vibaya madaraka”.

Taarifa hiyo inahitimisha kuanguka kwa aina yake kwa kardinali huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa na kumekuja kabla ya mkutano wa Vatican utakaofanyika Februari 21-24, ukihusisha maaskofu kutoka kila kona ya dunia kujadili namna ya kulinda watoto ndani ya kanisa.

Kashfa za ngono duniani, na hasa hivi karibuni katika nchi za Marekani na Chile zimeyumbisha Kanisa Katoliki na kumfanya Papa Francis kuahidi kuwa na sera isiyovumilia makosa hayo, hata kwa viongozi wa juu wa kanisa.

McCarrick, askofu mkuu wa zamani wa Washington, alizuiwa kufanya shughuli za kipadri Julai mwaka jana, baada ya kujivua ukardinali wake wa heshima. Kwa sasa anaishi Kansas.

McCarrick anajulikana kwa kufanya ngono na waseminari ambao ni watu wazima kabla ya kukumbwa na kashfa hiyo ya kumbaka mtoto mdogo.

Mwaka jana, waendesha mashtaka wa jimbo la Pennsylvania, Marekani walibaini kuwa viongozi wapatao 300 wa dini walihusika katika kashfa za kubaka watoto kuanzia miaka ya arobaini, lakini kashfa hizo zilifunikwa na maaskofu kadhaa.

Waendesha mashtaka katika majimbo mengine wameahidi kufanya uchunguzi kama huo.

Mwaka jana, Papa alikubali kujiuzulu kwa maaskofu kadhaa wa Chile baada ya uchunguzi kubainisha vitendo kadhaa vya uzinzi vilivyofanywa na viongozi hao wa dini.

Machi mwaka 2015, Papa alimruhusu Keith O’Brien kuendelea na ukardinali baada ya askofu huyo wa zamani wa Edinburgh na kiongozi wa zamani wa Kanisa Katoliki nchini Scotland kujiuzulu kwa tuhuma za uzinzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com