Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKUBWA YAIBUKA KIFO CHA RUGE MUTAHABA

Wengi walimfahamu Ruge Mutahaba kama mdau mkubwa wa burudani, lakini kifo chake kimeibua mengi makubwa aliyofanya nje ya nyanja hiyo.

Kutoka siasa, ujasiriamali, michezo, afya, mazingira, uchumi, utafutaji fursa hadi kujenga fikra chanya za maisha ni mambo yaliyoibuka baada ya kifo chake kilichotangazwa juzi jioni.

Hayo yamo katika salamu za rambirambi, mahojiano na watu mbalimbali waliofika nyumbani kwao Mikocheni kuomboleza, taarifa za vyombo tofauti vya habari na watu walioandika katika mitandao ya kijamii kuhusu maisha ya Ruge.


Ruge, mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, alifariki akiwa hospitalini nchini Afrika Kusini alikopelekwa kutibiwa takriban miezi minne iliyopita. Awali alipata matibabu nchini India.


Miongoni mwa waliotuma salamu na kufika nyumbani kutoa pole ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amemtaja Ruge kuwa nguzo iliyosimamisha uelekeo wa vijana wa sasa.


Alisema Ruge aliwasaidia vijana kwa kuwapa mwanga wa kutimiza ndoto zao.


Hivyo ndivyo anavyomzungumzia January Makamba, ambaye ni Waziri wa Mazingira, Hamisi Kigwangalla (Maliasili na Utalii), Antony Mtaka (mkuu wa Mkoa wa Simiyu) na wengine waliowahi kufanya kazi na Ruge.


Waziri Mkuu alisema Ruge amefanya kazi kubwa tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ya ujenzi wa Taifa, hasa katika kunyanyua vijana.


“Pia ametoa mchango wake wa mali kuwasaidia Watanzania hasa vijana,” alisema Waziri Mkuu.


“Tumempoteza kijana wetu na wito wangu kwa Watanzania wote tuungane kwa pamoja kumuombea ndugu yetu Ruge.”


Naye Kigwangalla amemsifu kwa kujitoa kwake katika shughuli za ujenzi wa Taifa, akisema ingawa alikuwa mgonjwa, Ruge alishiriki kikamilifu kuiandaa programu maalumu ya utalii inayoitwa Tanzania Unforgettable.


“Ni mtu ambaye alijijengea jina kubwa katika tasnia ya habari, maendeleo, uchumi na burudani kwa ujumla,” amesema.


Alisema heshima hiyo ameipata kutokana na uwezo wake wa kubuni vitu mbalimbali, kiasi cha watu kudiriki kusema alikuwa injini ya Clouds.


“Ruge alifanya kazi kwa bidii usiku na mchana hata alipokuwa anaumwa,” alisema.


“Siku moja kabla ya mimi kupata ajali (Agosti 3,2018), tulikuwa Arusha na licha ya yeye kuwa India anaumwa, aliporejea nchini hata kabla hajaripoti kazini kwake alikuja Arusha na alishiriki kikamilifu.


“Ruge alikuwa mtetezi sana wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wadau wa utalii. Alijitoa sana kwa kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na wadau na kwa kiasi kikubwa ameshiriki Tanzania Unforgettable kikamilifu.”


Naye Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson alimmwagia Ruge sifa kutokana na ubunifu, akisema asilimia kubwa ya mawazo ya kuanzishwa kwa taasisi ya Tulia Trust ni yake.


Alisema ni mtu aliyekuwa akiwapa moyo vijana na kuwataka watu wanaomlilia, waishi katika maneno yake.


“Nimepokea msiba wake kwa shukrani na huzuni kwa kuwa ni mtu ambaye alikuwa na mchango kubwa kwa watu wengi,” alisema Dk Tulia.


“Ni mtu ambaye ulikuwa unampigia simu na kumuomba mawazo yake, hivyo unafikiria leo mtu kama huyo hayupo, unawaza namna ya kutafuta rafiki mwingine wa aina yake.”


Waziri Ummy alisema amepata pigo kwa kuwa mikakati aliyokuwa nayo Ruge katika kuiboresha sekta ya afya nchini ni mikubwa.


Ummy alisema Ruge aligusa maisha ya wengi hasa vijana katika masuala mbalimbali hususani kufikisha ujumbe katika jamii hasa katika masuala ya afya ya uzazi kwa vijana na mapambano dhidi ya VVU.


Alisema katika kipindi cha uhai wake, Ruge alishirikiana na Serikali katika kufanya kampeni za masuala ya afya, kama ya Malaria na Nyumba ni Choo.




Pengo lake katika siasa


Mbali na masuala hayo, Ruge amezungumziwa kwa mtazamo chanya na vyama vya siasa, akielezewa kama mtu aliyeweka jukwaa la kukuza demokrasia na kupigania uhuru wa habari nchini.


Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali alisema Ruge alirahisisha shughuli za ujenzi wa chama hicho kupitia majukwaa mbalimbali ya vijana.


“Hata wakati wa kampeni za uchaguzi, mchango wake ulikuwa mkubwa kwa sababu vipindi vilivyokuwa vinaandaliwa vilikuwa vinaboresha demokrasia,” alisema Dk Bashiru.


“Kwa kuwa kipindi cha uchaguzi huwa kuna hamasa kubwa, tukikosa watu wabunifu inaweza kuwa balaa. Kwa hiyo aliunganisha watu na sera.”


Naye katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema Ruge alithubutu kuweka usawa katika jukwaa kwa vyama vya siasa kuuza sera zao katikati ya mazingira magumu ya uhuru wa vyombo vya habari.


“Pamoja na hali ya kidemokrasia na uminyaji wa vyombo vya habari, Ruge aliweza kutukaribisha na kutupatia jukwaa la kutangaza ajenda zetu kwa wananchi, tofauti na vyombo vingine vingi tu. Nilishiriki kipindi cha live 360. Ni uaminifu mkubwa sana alioonyesha kwa chama,” alisema.


“Kwa hiyo tumepata msiba, tasnia ya habari hususani upande wa vijana, itakuwa imeyumba sana. Kama chama tumepokea kwa masikitiko sana kifo chake, tunamwombea kwa Mungu ampumzishe kwa amani.”


Dk Mashinji amesema Ruge alitamani kuona wanasiasa wakishiriki siasa safi.


Ruge alitamani kuona uhuru wa habari ukiheshimiwa nchini.


“Nakumbuka hadi Clouds inavamiwa studio zake, alionyesha ujasiri na akaonyesha msimamo wa kutoyumbishwa katika uhuru wa habari. Kwa hiyo ni pengo kubwa sana kwa Taifa na tasnia ya wanahabari,” alisema.




Wanamichezo wamlilia


Ruge hajaliliwa na wanasia na wasanii pekee; bali hata wanamichezo.


Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah (Try Again) amemuelezea Ruge kuwa alikuwa mwanachama na mchezaji wa timu ya kundi la Friends of Simba na Simba Veterans.


“Amewahi kushiriki kuandaa sherehe ya Simba Day, vilevile niliwahi kumshauri aanzishe kampuni akanisikiliza na ndiye alinipa jina la Try Again ambalo linanitambulisha katika soka,” alisema Try Again.


“Ruge alikuwa na mchango mkubwa sana kwenye klabu yetu, alikuwa mjumbe wa kamati ya Masoko na Uwekezaji ya Simba,” alisema.


“Nikiwa mwenyekiti wa hiyo kamati, tumefanya naye mambo mengi ikiwamo kuandaa moja ya sherehe za Simba Day.”


Naye kaimu mwenyekiti wa Yanga, Samwel Lukumay alisema kifo cha Ruge ni pigo kwa Taifa kwa kuwa alikuwa na ushawishi na mchango mkubwa kwa vijana.


“Nakumbuka kuna mechi moja ya Simba na Yanga, Ruge alikuwa mstari wa mbele katika kuitangaza na ikateka nchi,” alisema.


Alisema mbali na mechi hiyo, Yanga ilikuwa ikishirikiana na Clouds Media katika matangazo na kupewa ushirikiano mkubwa na Ruge.


Naye bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 1500 na mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki ya 1980, Filbert Bayi alisema vijana wanapaswa kujifunza kutokana na kile alichokifanya Ruge katika tasnia tofauti.


“Wakiendeleza yale mazuri ambayo Ruge ameyafanya enzi za uhai wake, itakuwa ni shukrani tosha katika kumuenzi kwa mazuri yake, kwa kuwa alikuwa ni mtu ambaye alijitoa,” alisema Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa TOC.


Upande wa masumbwi pia walikuwa na kilio chao.


“Binafsi Ruge amenisimamia mapambano yangu kama matatu, hakuishia hapo hata mdogo wangu Mbwana ameandaliwa mapambano mengi tu na Ruge,” alisema nyota na bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla.


“Alikuwa kijana mwenye mipango mingi ya maendeleo katika tasnia mbalimbali.” Bondia Francis Cheka alisema kwa mara ya kwanza pambano alilopigana kwenye ngumi za kulipwa na kupata fedha nyingi liliandaliwa na Prime Time Promotions ambako Ruge alihusika.


Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com