SERIKALI imekabidhi rasmi eneo la mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (RHPP), kwa mkandarasi Kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na ile ya Elsewedy Electric zote kutoka nchini Misri.
Hatua hiyo sasa inaashiria kuanza kwa kazi ya ujenzi wa mradi huo wa umeme ambao utazalisha Megawati 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye dridi ya Taifa na kuifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.
Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alikabidhi mradi huo jana katika eneo la Hifadhi Matambwe lililopo mpakani mwa mikoa ya Pwani na Morogoro, akisema faida nyingine ya mradi huo utakapokamilika bei ya umeme itashuka kwa kiwango kikubwa na utasaidia nchini kutekeleza rasilimali muhimu za Taifa.
Alisema mradi huo utajenga bwawa kubwa, lenye mita za ujazo bilioni 34 na kituo cha kufua umeme, kitakachokuwa na mashine tisa za kuzalisha umeme zenye uwezo wa megawati 2,115.
Aidha, alisema pindi mradi huo ukikamilika, utasaidia kushusha gharama za umeme kutokana na uzalishaji wa umeme huo wa kutumia maji kuwa nafuu, tofauti na nishati nyingine kama mafuta, gesi, upepo na jua.
Aliwataka wakandarasi hao, kukamilisha mradi huo kwa muda waliokubaliana, huku akiwapongeza wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuchangia utekelezaji wa mradi huo kwa hatua za awali.
Aliwataka wakandarasi watakaotekeleza ujenzi huo, kujenga kwa ufanisi mkubwa na kwa viwango vinavyotakiwa na muda uliopangwa na utakaondoa shaka kwa wale wasioutakia mema mradi huo.
Dk Kalemani alimpongeza Rais John Magufuli kwa jinsi ambavyo amechukua ujasiri wa kuamua kutekeleza ndoto za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye mwaka 1958 alikuwa na mpango wa kujenga bwawa hilo, lakini ikashindikana kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo za kifedha.
Hivyo aliwataka wakandarasi wa kampuni hizo na timu ya wataalamu wa Tanesco, kutoondoka eneo la mradi baada ya kukabidhiwa eneo, kwa kuwa hadi sasa kila kitu kipo kuanzia nyumba za kuishi, umeme na maji. Aliwataka wajenge wakati wote wa mvua na jua.
“Hatutaki kugeuka nyuma kuanzia sasa, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco ushiriki kikamilifu ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa,” alisema Dk Kalemani.
Aliongeza, “Mimi na Naibu Waziri na hata Rais tutakuwa bega kwa bega usiku na mchana kuona mradi unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa viwango na ubora wa kimataifa wa mabwawa ya kufua umeme.”
Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaleta tija katika kujenga uchumi wa nchi kupitia sekta ya viwanda. Alisema mahitaji ya umeme nchini kwa sasa ni makubwa kwani nchi inatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo huduma za umeme wa uhakika inahitajika zaidi.
Dk Kalemani alisema ujenzi wa mradi huo, unajumuisha ujenzi wa bwawa kuu lenye uwezo wa kutunza maji takribani mita za ujazo bilioni 34, kituo cha kufua umeme kitakachokuwa na mashine tisa za kuzalisha umeme zenye uwezo wa megawati 235 kila moja, hivyo kufanya uwezo kuzalisha umeme wa mradi megawati 2,115.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema mradi huo wa kihistoria, uliosainiwa kati ya Tanesco na Kampuni ya Ubia Arab Contractors (Osman A. Osman Co na Elsewedy Electric), utakuwa na mkataba wa miezi 42.
Msimamizi Mkuu wa kampuni mbili zilizopewa kandarasi hiyo, Makamu wa Rais wa kampuni hizo kutoka Serikali ya Misri, Wael Handy alisema mradi huo si wa Watanzania pekee, bali ni faida kwa wananchi wa Afrika yote.
Alisema mradi huo umeshirikisha timu mbalimbali za wataalamu wa sekta mbalimbali na katika kutekeleza mradi huo, Serikali ya Misri haitawaangusha na itahakikisha unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.