Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Janturu maarufu Mtaturu (40 -45) mkazi wa Katunda Mjini Shinyanga amefariki dunia muda mfupi baada ya Mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC na Al Ahly kwenye mchezo wa Kundi D jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Jamaa huyo anayedaiwa kuwa shabiki damu wa Simba SC amefariki dunia ikielezwa kuwa alikuwa akishangilia ushindi wa Simba SC ambayo imewafunga Al Ahly bao 1-0.
Mashuhuda wa tukio wameiambia Malunde1 blog kuwa shabiki huyo wa Simba SC alikuwa na furaha kupita kiasi baada ya timu yake kupata bao hilo.
“Huyu jamaa ni Muuza Nyama duka lake limeandikwa Mtaturu Butcher,lipo kona ya Buhangija.. Ni Mpenzi sana wa Simba SC, alikuwa kwenye kibanda cha kuangalizia mpira karibu na Stand ya Mabasi Ibinzamata,baada ya Simba SC kupata bao la kwanza,alichukua nguo nyekundu ya Simba na kulazimisha kumvalisha mtani wake shabiki wa Yanga,lakini shabiki huyo wa Yanga aliichana hiyo nguo,
…mpira ulipomalizika ukatokea mzozo flani hivi akidai nguo yake iliyochanwa ,hata hivyo hawakupigana, baada ya hapo jamaa aliondoka kibandani, hatua kadhaa akaanguka na kuanza kutoa mapovu,amefariki akipelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga”,wanaeleza mashuhuda wa tukio hilo.
Inaelezwa kuwa jamaa huyo ni shabiki damu wa Simba SC,na timu yake hiyo ilipofungwa bao 5-0 na Al Ahly hakuwa na raha takribani siku tatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule ameiambia Malunde1 blog kuwa bado hajapata taarifa kuhusu tukio na kuahidi kutoa taarifa baadaye.
Social Plugin