Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AL AHLY WAIPIGA 'KHAMSA ' SIMBA SC ... NI KICHAPO CHA MBWA KOKO

Simba SC imepoteza mechi ya pili mfululizo ya ugenini ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 5-0 na wenyeji, Al Ahly katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria nchini Misri.

Kipigo hicho kinafuatia kipigo kingine cha 5-0 kutoka kwa AS Vita kwenye mchezo uliopita Januari 19 dhidi ya AS Vita mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Tofauti tu ni kwamba, Januari 19 mjini Kinshasa Simba ilifungwa mabao matatu kipindi cha kwanza na mawili kipindi cha pili, lakini imeruhusu mabao yote hayo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza pekee.
Amr Al Sulaya alianza kufunga la kwanza dakika ya tatu akimalizia pasi ya Hussein El Shahat, kabla ya Ali Maaloul kufunga la pili dakika ya 23 akimalizia pasi ya Nasser Maher.

Maaloul akamsetia Oluwafemi Junior Ajayi kufunga bao la tatu dakika ya 31, kabla ya Karim Nedved kufunga mabao mawili, dakika ya 33 na 40, mara zote akimalizia pasi nzuri za kiufundi za Hussein El Shahat.

Kipindi cha pili Simba SC waliingia kucheza kwa kujihami kujizuia kuruhusu mabao zaidi na wakafanikiwa kumaliza dakika 90 wakiwa wamechapwa mabao 5-0 tu.

Mchezo mwingine wa Kundi D leo, wenyeji AS Vita wamelazimishwa sare ya 2-2 na JS Saoura Uwanja wa Martyrs de la Penteccte mjini Kinshasa.

AS Vita watajilaumu wenyewe, kwani waliuanza vizuri mchezo huo na kuongoza 2-0 hadi dakika ya 37 kwa mabao ya Kazadi Kasengu dakika ya 14 na Jean-Marc Makusu Mundele, wote wakimalizia pasi za Tuisila Kisinda, lakini wakajiruhusu kusawazishiwa. 

Mohamed El Amine Hammia alianza kufunga kwa penalti dakika ya 45 kabla ya Sid Ali Yahia Chérif kusawazidha dakika ya 88.
Sasa Al Ahly inaendelea kuongoza Kundi D kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na AS Vita pointi nne, SImba SC pointi tatu na JS Saoura pointi mbili.

Mechi zijazo Februari 12 Simba watakuwa wenyeji wa Al Ahly kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na JS Saoura watawaakribisha AS Vita Saa 4:00 usiku nchini Algeria.
Kikosi cha Al Ahly kilikuwa; Mohamed El Shenawy, Ayman Ashraf/ Rami Rabia dk79, Saad Samir, Ali Maaloul/dk59, Mahmoud Waheed, Mohamed Hany/ Hossam Ashour dk71, Hesham Mohamed, Amr Al Sulaya, Karim Nedved, Hussein El Shahat, Nasser Maher na Oluwafemi Junior Ajayi.

Simba SC; Aishi Manula, Serge Wawa, Juuko Murshid, Asante Kwasi, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk56, James Kotei, Clatous Chama/Hassan Dilunga dk82, Meddie Kagere/John Bocco dk74, Emmanuel Okwi, Rashid Juma na Nicholas Gyan.

Via>>Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com