Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania, klabu ya Simba wamefanikiwa kuvunja mwiko wa kutoshinda kwenye uwanja wa Samora Mjini Iringa dhidi ya Lipuli FC, kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Simba imepata ushindi huo kwenye mchezo wa ligi kuu, ambapo mabao mawili ya Simba yamefungwa na Clatous Chama huku moja likifungwa na Meddie Kagere ambaye sasa ameanzisha vita ya mabao na mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo ambpo sasa wamefungana kwa mabao 12.
Kagere ambaye amefunga katika mechi 4 mfululizo za Simba, sasa anasimama katika nafasi ya pili ya wafungaji msimu huu akiwa na sawa na Makambo huku wakizidiwa na Salum Aiyee wa Mwadui FC mwenye mabao 13.
Kwa ushindi wa leo Simba sasa wamefikisha pointi 48, katika michezo 19, wakiendelea kusalia katika nafasi ya 3 wakiwa nyuma ya Azam FC yenye alama 50 wakati vinara Yanga wakiwa na alama 61.
Baada ya mechi ya leo Simba wanasafiri kuelekea Kanda ya Ziwa mkoani Shinyanga kucheza na Stand United wakati Yanga nao watakuwa huko huko jijini Mwanza wakisubiri kukipiga na Alliance FC, hivyo vita ya mabao ya Makambo na Kagere ikitarajiwa kupata kinara endapo watafunga.
Social Plugin