Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TPDC YAIMARISHA SEKTA YA ELIMU MKOANI MTWARA


Bi. Marie Msellemu, Meneja Mawasiliano wa TPDC akimkabidhi hundi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mh. Bw. Gelasius Byakanwa kiasi cha Tsh,. 13, 258,042 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa Mkoani Mtwara.
Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hundi kwa mratibu wa tasisi ya TAKUWA Bi. Hadija Malibecha 
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Ndg.Omari Kipanga akitoa ufafanuzi wa mahitaji ya elimu mkoani Mtwara.
 ***
Katika jitihada za kutekeleza dhana ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kutekeleza kwa vitendo dhana hii kwa kushiriki katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo Mkoani Mtwara. 

Katika tukio la hivi karibuni, TPDC imeweza kumkabidhi Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mh. Bw. Gelasius Byakanwa hundi ya kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu laki mbili hamsini elfu na arobaini na mbili ili kusaidia ujenzi wa darasa moja katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara. 

Akiongea katika tukio hilo, Mh. Byakanwa alisema TPDC imefanya jambo kubwa na kuonyesha uzalendo kwa kurudisha kwa jamii, na aliishukuru TPDC kwa kuendelea kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali mkoani Mtwara, husani zile zinazoikumba sekta ya huduma za jamii ikiwemo elimu. 

Vile vile mkuu wa mkoa alitoa rai kwa wadau na wawekezaji waliopo mkoani Mtwara kuiga mfano wa TPDC katika kuwajali wananchi kwa kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akimkabidhi mfano wa hundi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Bi. Marie Msellemu ambaye ni Meneja Mawasiliano wa Shirika alisema..

 “TPDC ni mdau mkubwa wa Mkoa wa Mtwara, na kwa kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), TPDC imekuwa ikiwashika mkono wananchi wa Mkoa wa Mtwara na mikoa ya jirani katika kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na hivyo kiasi hiki cha fedha kitauwezesha mkoa kuendelea kufikia lengo la kuweka mazingira mazuri ya kusomea kwa watoto wetu”. 

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Ndg. Omari Kipanga alieleza kuwa..

 “Sisi kama halmashauri tumefarijika sana kwa msaada huu uliotolewa na TPDC, kwani fedha hizi zitaelekezwa moja kwa moja katika ujenzi wa madarasa katika halmashauri ya Wilaya yetu kama ilivyokusudiwa. Mchango huu uliotolewa na TPDC unakwenda kukamilisha kazi ya kuezeka madarasa manne katika shule ya msingi Mitambo pamoja na madarasa mawili katika shule ya sekondari ya Madimba’’. 

Mkurugenzi Kipanga aliendelea kusisitiza kwamba uhitaji bado ni mkubwa kuweza kukamilisha uhitaji wa madarasa kwa Mkoa wa Mtwara na kuwataka wadau wa elimu na wawekezaji mbalimbali waliopo mkoani Mtwara kuiga mfano wa TPDC katika kurudisha kwa jamii na kuimarisha elimu mkoani hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndg. Evod Mmanda naye aliungana na viongozi waliotangulia kwa kuishukuru na kuipongeza TPDC kwa kusaidia kuboresha huduma mbali mbali za kijamii mkoani Mtwara. 

Alieleza kuwa...

 “Si mara ya kwanza kwa TPDC kuchangia kwani mwaka jana tumepokea kiasi cha 21,151,500 za kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijjiji cha Mngoji pamoja na kiasi cha 12,000,000 za ujenzi wa choo cha wanafunzi wenye uhitaji maalumu katika shule ya msingi Shangani”. 

Katika hatua nyingine TPDC ilikabidhi Taasisi ya Kusaidia Wanawake Mkoani Mtwara (TAKUWA) kiasi cha milioni tatu laki tisa na elfu sabini kwa ajili ya unununuzi wa vitendea kazi vya ofisi ili kurahisisha shuguli za kila siku za taasisi hiyo. 

Mratibu wa taasiis hiyo Bi. Hadija Malibecha alishukuru TPDC kwa msaada huo na alieleza kuwa “kabla ya upatikanaji wa vifaa hivyo tulikua tunafanya kazi katika mazingira magumu lakini sasa TPDC imetuboreshea mazingira ya kazi na kazi zinaenda vizuri”. TAKUWA inasaidia vikundi vya wanawake kwa ajili ya kuinua shughuli mbalimbali za kiuchumi na elimu. 

Jumla ya vikundi 12 vya wakinamama mkoani mtwara vinasimamiwa na taasisi hii katika kupewa mafunzo ya ujasiriamali kama kutengeneza sabuni, ufugaji wa nyuki na ufugaji wa wa mbuzi lengo ikiwa ni kuboresha maisha ya wanawake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com