Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mkutano wake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un utafanyika baadae mwezi huu, kwenye mji mkuu wa Vietnam, Hanoi.
Trump ameandika leo katika ukurasa wake wa Twitter kwamba wawakilishi wake wameondoka Korea Kaskazini baada ya kufanya mazungumzo yaliyofanikiwa na wamekubaliana kuhusu muda na siku ya kufanyika kwa mkutano huo wa kilele kati yake na Kim.
Amesema mkutano huo wa pili kati ya viongozi hao utafanyika Februari 27 na 28, Trump na Kim walikutana kwa mara ya kwanza mwaka uliopita huko Singapore.
Trump amebainisha kuwa Korea Kaskazini chini ya uongozi wa Kim, itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi. Kiongozi huyo wa Marekani amesema amejiandaa kukutana na Kim ili kuendeleza mchakato wa amani.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa mjumbe maalum wa Marekani nchini Korea Kaskazini, Stephen Biegun atakutana tena na maafisa wa Korea Kaskazini kabla ya mkutano wa Trump na Kim.
Biegun amewasili Seoul, Korea Kusini akitokea Pyongyang baada ya kufanya ziara ya siku tatu ambako alijadiliana na maafisa wa Korea Kaskazini kuhusu mkutano wa viongozi hao.
Social Plugin