Mbunge wa Jimbo la Ushetu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amekemea vitendo vya kiuhalifu vinavyoendelea katika Halmashauri ya Ushetu ambavyo vimepelekea kusababisha majeruhi na vifo kwenye Halmashauri hiyo.
Amezungumza hayo katika kata ya Mpunze iliyopo katika Halmashauri hiyo ambapo kabla ya kuzungumza nao Mbunge huyo alipita katika kituo cha afya cha Ukune kwa ajili ya kuitizama na kuipa pole familia moja iliyoivamiwa usiku na kikundi cha watu kisichojulikana ambacho kiliwashambulia familia hiyo kwa kukatwa mapanga na kuwaibia fedha.
Mbunge Kwandikwa, ameonesha kusikitishwa na matukio yanayoendelea katika kata hizo na kuwaahidi wananchi wake kulisimamia suala hilo kikamilifu.
"Hatuwezi kukubali hali hii kwasababu wananchi wanaogopa kufanya biashara na wengine wanaogopa kuzalisha hivyo suala la ulinzi lipo mikononi mwetu wenyewe ni lazima jambo hili tuliondoe", amesisitiza Mbunge Kwandikwa.
Ameongeza kuwa atafanya juhudi za kuweka Kituo cha Polisi maeneo jirani ili kuweza kuongeza hali ya usalama kwa wananchi na iwe rahisi kwao kuripoti kituoni hapo matukio yote ya kiuhalifu pindi yanapotokea.
Aidha, Mheshimiwa Kwandikwa, amewataka wananchi kutoa taarifa kwake na kwa vyombo vya usalama kwa yeyote wanayemdhani anajihusisha na vitendo vya kijambazi katika maeneo yao ya wanamoishi.
"Hatutovumilia hali hii naomba viongozi wanaouhusika na ulinzi mjipange kisawasawa kwani hata mimi saa hii niko tayari kazini", amefafanua Mbunge huyo.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo amewaeleza wananchi wake baadhi ya miradi inayoendelea kufanyika katika kata hiyo na kata zingine za Halmashauri ya Ushetu na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu na kujitoa katika shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sabasabini, Bw. Emmanuel Makashi, amemshukuru Mbunge huyo kwa kulisimiamia suala la usalama katika kata za jimbo lake kwani limekuwa kero ambapo naye ni miongoni mwa waathirika wa kuvamiwa.
Mbunge huyo yupo mkoani Shinyanga kukagua hatua zilizofikiwa katika miradi inayoendelea kutekelezwa kama vile ujenzi wa hospitali ya wilaya, jengo la halmshauri, na barabara zinazoendelea kujengwa kwa kiwango cha changarawe ya Nyamilangano-Butibu yenye urefu wa kilomita 12.
Chanzo - Habarileo
Chanzo - Habarileo