Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : TVMC YAFADHILI VIJANA KUSOMA CHUO CHA MAENDELEO YA WANANCHI,YAKABIDHI VIFAA MUHIMU


Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC) linalotoa huduma za kijamii kwa upande wa vijana ,watoto na wanawake na makundi yasiyojiweza limewafadhili vijana watano wa kike kuendelea na masomo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga.

Vijana hao ambao wameshindwa kuendelea na masomo katika mfumo rasmi baada ya kuhitimu masomo ya darasa la saba mwaka 2018 wanatoka katika kata ya Chamaguha katika Manispaa ya Shinyanga.

Shirika la TVMC limewalipia ada na kuwapatia mahitaji yote muhimu yanayotakiwa chuoni vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 3.4 lengo likiwa ni kupambana na mimba na ndoa za utotoni.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa vya wanafunzi hao kisha kuwakabidhi wahusika leo Jumatatu Februari 4,2019, Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Octavina Kiwone alisema TVMC imefanya jambo jema ili kuwasaidia vijana kujiendeleza kielimu hali itakayowafanya wajikwamue kimaisha.

“Tunawashukuru TVMC kwa kuwa wadau muhimu katika manispaa yetu,mmekuwa pamoja na watoto hawa tangu mwaka 2016 kwa kuwapatia huduma mbalimbali ikiwemo kuwapa sare za shule na kuwalipia bima za afya,tunaimani vijana watatumia fursa hii kusoma kwa bidii na kutokubali kurubuniwa”,alieleza Kiwone.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TVMC, Mussa Ngangala ufadhili huo wa masomo kwa vijana wanaotoka katika mazingira magumu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni unaotekelezwa na TVMC kwa ufadhili wa shirika la Firelight Foundation la nchini Marekani.

“Vijana hawa wameshindwa kuendelea na masomo katika mfumo rasmi,hivyo tumeona ni vyema kuwaendeleza kielimu kwani elimu hii itawasaidia kuendeleza maisha yao,na hawa watano tuliowapeleka chuoni watakuwa mfano kwa wengine na tunatarajia kuongeza wengine kadri tutakavyopata nafasi”,alisema Ngangala.

“Vijana hawa watapata mafunzo mbalimbali kwenye chuo cha FDC Buhangija kwa muda wa mwaka mmoja,tumewalipia ada shilingi 500,000/= kila mmoja na kuwapatia mahitaji yote muhimu chuoni kama vile magodoro,vyandarua,vyombo,shuka na vifaa vya kujifunzia”,alieleza.

Aidha aliishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na shirika hilo katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wao,vijana hao walilishukuru shirika hilo kwa kuwashika mkono na kuahidi kuzingatia masomo yao chuoni.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Octavina Kiwone akizungumza wakati Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC) likikabidhi vifaa kwa vijana watano ambao wamefadhiliwa na shirika hilo kujiunga na masomo katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Octavina Kiwone akiwasisitiza vijana kuzingatia masomo yao huku akiwataka wazazi na walezi kutowatenga watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC), Mussa Ngangala akizungumza wakati akikabidhi magodoro na vifaa mbalimbali kwa vijana watano ambao wanajiunga katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC), Mussa Ngangala (kulia) akimuonesha vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto/vijana watano wanaojiunga katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija. Kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Octavina Kiwone.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC), Mussa Ngangala akionesha kifaa cha kujifunzia katika chuo cha FDC.
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Octavina Kiwone akipokea godoro kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC), Mussa Ngangala kwa ajili ya vijana wanaofadhiliwa na shirika hilo.
Vijana wakibeba vifaa vyao na kuviweka kwenye gari kwa ajili ya safari kuelekea katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com