Waganga wa tiba asili waliopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wamepewa siku 16 kuhakikisha kila mmoja anakuwa na kitambulisho cha wajasiriamali kilichotolewa na Rais John Magufuli.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga wakati akiongea na viongozi wa waganga hao mkoa, alipokutana nao kujadili namna bora ya kuboresha kazi zao.
Kiswaga amesema kuwa katika wilaya hiyo kuna waganga wa tiba asili 600, na kwamba mganga yeyote ambaye hatakuwa na kitambulisho hicho baada ya siku hizo kuisha atafutiwa leseni yake na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hadi kufikia Februari 20, mwaka huu kila mganga wa jadi awe na kitambulisho hicho, usipokuwa nacho tutakunyang’anya leseni yako kukuzuia kuendelea kufanya kazi zako, baada ya muda huo,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waganga hao, Samson Maduhu amesema ndani ya muda huo waganga wote 600 wanafikiwa na kupatiwa vitambulisho hivyo.
Social Plugin