Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia raia 13 wa Ethiopia wakiwa wamejificha kwenye shamba la mkazi mmoja wa mtaa wa Nyaburogoya Kata ya Nyegezi jijini Mwanza.
Miongoni mwao, watano wamekutwa na hati za kusafiria zilizotolewa na Ethiopia zilizogongwa muhuri na Idara ya Uhamiaji ya Kenya, lakini bila kugongwa mhuri na idara hiyo nchini.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro, alisema watu hao walikamtwa Februari 13, mwaka huu asubuhi, kufuatia taarifa za kiintelijensia kutoka kwa raia wema, na kwamba walipofuatilia walikuta ni kweli kisha kuwakamata13, ambao walitambulika kuwa ni raia wa nchi hiyo.
“Tunachoendelea nacho kwa sasa ni kutaka kujua hawa watu wamefikaje hapa nchini, wamesafirije hadi kupita mpakani na ni nani mwenyeji,” alisema Kamanda Muliro na kuongeza:
“Watakapobainika wanaowapatia mbinu za kuingia nchini bila vibali watachukuliwa hatua sitahiki za kisheria, ikiwamo kufikishwa kwenye vyombo husika.”
Aidha, alisema kutokana na watu hao kutokuelewa lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, utaratibu unafanyika wa kumtumia mkalimani ili kubaini sehemu wanayotoka na wanapokwenda.
“Tunawashikilia katika kituo kikuu cha Nyamagana, taratibu zinafanyika za kuwafikisha katika idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria,” alisema.