WANAWAKE WASIOHUDHURIA KLINIKI WATAJWA KUCHANGIA WATOTO KUZALIWA NA MATATIZO YA KIAFYA



Kadi ya kliniki 

Na Annastazia Paul - Shinyanga 

Imeelezwa kuwa ipo haja ya akina mama kuanza kliniki mapema mara tu wanapogundua kuwa ni wajawazito ili kuwezesha kuzaliwa watoto wenye afya njema ili kukabiliana na changamoto ya watoto kuzaliwa na matatizo ya kiafya.

Hayo yamesemwa jana na Afisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga,Denis Madeleke wakati akizungumza na Malunde 1 blog ambapo amebainisha kuwa kutokuhudhuria kliniki kwa wakati kwa akina mama wajawazito kunachangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya kiafya 

Aliyataja matatizo hayo ya kiafya kuwa ni pamoja na kichwa kikubwa na mgongo wazi pamoja na magonjwa mangine yanayosababishwa na lishe ambayo husababisha watoto kudumaa. 

Alieleza kuwa kliniki ndipo mahali ambapo mama mjamzimto atapatiwa elimu juu ya masuala mbalimbali yatakayomuwezesha kuwa na afya njema katika kipindi chote cha ujauzito na pia kusaidia kuzaliwa kwa mtoto mwenye afya njema. 

“Tunashauri pale tu mama anapojihisi mjamzito ahudhurie kliniki mara moja ili aweze kupewa huduma mbalimbali ambazo wanapewa akina mama wajawazito kwa mfano kuna dawa za kuongeza damu anatakiwa azipate ili kuepuka madhara kwa mtoto ambayo yanaweza kumpata kutokana na mama kutokutumia dawa hizo”,alisema. 

Alifafanua kuwa mama asipotumia dawa za kuongeza damu katika kipindi cha mwanzo cha ujauzito anaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tatizo la mgongo wazi au kichwa kikubwa, na kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa wajawazito kwenda kliniki mapema. 

Dk. Madeleke aliongeza kuwa mama anapohudhuria kliniki anapata nafasi ya kupewa elimu ya lishe bora ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa mtoto mwenye afya njema kwani virutubisho vingi vinavyojenga mwili wa mtoto vinapatikana kwenye chakula. 

“Pia ili kuepusha tatizo la magonjwa ya watoto yanayosababishwa na lishe duni kama vile, atapiamlo ukondefu na hata udumavu kwa watoto, ni lazima mama mjazito ale chakula mchanganyiko chenye virutubisho vyote vinavyotakiwa mwilini kwa kuzingatia makundi matano ya chakula”,alisema. 

“Mama mjamzito anatakiwa azingatie lishe bora ili aweze kutuletea mtoto mwenye afya njema, na anahitaji kula mlo mchanganyiko kwani tuna vyakula vya makundi matano”,aliongeza Afisa Lishe huyo. 

Aidha aliishauri jamii kuondokana na dhana potofu ya kuona kuwa kazi ya kulea ujauzito pamoja na mtoto anapozaliwa ni ya mama pekee bali wanaume wanatakiwa kushirikiana kwa pamoja katika malezi ili kusaidia makuzi bora ya mtoto. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post