Mbunge wa Kimilili nchini Kenya Didmus Barasa amemwandikia Spika wa Bunge Justin Muturi akitaka aongezewe walinzi kwa sababu anadai maisha yake yapo hatarini.
Akihutubia wanahabari Alhamisi katika majengo ya Bunge, jijini Nairobi Bw Barasa alisema amekuwa akipokea simu na jumbe za kutisha kutoka kwa watu wasiojulikana wakitaka kumuua.
“Katika barua hizo wamekuwa wakiniambia kwamba… 'Tunataka kichwa chako kidogo na viungo vingine vya mwili wako, nyamaza na ukome kutangatanga’,” alisema.
Mbunge huyo wa chama cha Jubilee alisema majuzi watu hao walijaribu kumteka nyara mwanawe wa kiume ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Consolata, Nairobi.
“Nilipata simu kutoka kwa mwalimu wa mtoto wangu akiniambia mwanaume fulani alikuja shuleni humo akidai ametumwa kumchukua mwanangu amrejeshe nyumbani.
Mwalimu aliposisitiza kunipigia simu kwanza, jamaa huyo akatoweka,” Barasa aliongeza kusema.
Kulingana naye, watu fulani wamekuwa wakivizia boma lake huko Kimilili na karibuni walipatikana wakitaka kuliangusha ili kuingia katika boma hilo kwa nguvu.
“Niliwahi kuripoti polisi kisa ambapo nilishambuliwa na watu wenye bunduki lakini nikaponea. Mtu mmoja alikamatwa na kesi hiyo bado inachunguzwana na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), Langata,” alisema.
Akiandamana na Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Laikipia Bi Catherine Waruguru, Barasa alidai kuwa mwanasiasa mmoja, ambaye hakumtaja, amekuwa akimtishia maisha.
Mbunge huyo alitoa wito kwa DCI katika eneo bunge la Kimilili na Nairobi kuharakisha uchunguzi kuhusu tisho kwa maisha yake.