Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU 28 MBARONI MATUKIO YA UTEKAJI NA MAUAJI YA WATOTO NJOMBE


Baadhi ya wafanyabiashara wa miji ya Njombe na Makambako mkoani Njombe ni miongoni mwa watu 28 wanaoshikiliwa na polisi wakituhusishwa  na mwendelezo wa matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yanayoendelea wilayani Njombe.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Renata Mzinga amesema leo Jumatatu Februari 04, 2019 ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya msako wa kubaini mtandao wa watu wanaojihusisha na matukio hayo.

Amesema pia waganga sita wanaodaiwa kujihusisha na matukio hayo wametiwa mbaroni na wanaendelea na mahojiano dhidi yao.

"Tunaendelea na msako mkali kwa kushirikiana na kikosi maalumu kutoka makao na hadi leo hii tunawashikilia watu 28 wakiwamo waganga wa jadi sita, wafanyabiashara na watu wengine wa kawaida," amesema.

Amesema matukio yote yaliyojitokeza ya mauaji, wamekamatwa watu kuhusiana na uhusika wao na vyombo vya dola vinaendelea na upelelezi wa kuwabaini wahalifu.

Kamanda huyo amesema wana taarifa za watuhumiwa waliokimbia wakiwamo waganga wa jadi lakini wameshajua walikokimbilia na vyombo vya dola vitawasaka popote hadi watiwe nguvuni.

“Tunaendelea kuwasihi wananchi wa Njombe waendelee kutoa ushirikiano wa kuwabaini wahusika wa mauaji ya watoto wadogo wasio na hatia,” amesema.

Na Godfrey Kahango, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com