Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango amekutana na Watumishi wa Wizara hiyo na kuzungumza nao namna bora ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ili kusukuma kasi ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Mpango alisema Wizara ya Fedha na Mipango ni kitovu cha Serikali hivyo Watumishi wote wa Wizara wanawajibu wa kutekeleza majukumu kwa kuzingatia nidhamu, maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ili kuongeza tija.
Amesema kila mtumishi anawajibu wa kufanya kazi kwa weledi, bidii na kushirikiana na kila mmoja katika nafasi yake ili kuboresha utendaji kazi na kukuza uhusiano mahala pa kazi.
Aidha Waziri Mpango aliwapongeza Watumishi wa Wizara hiyo kwa kazi wanazozifanya hususan kazi ya uandaaji wa Bajeti Kuu ya Serikali, Uchambuzi wa Sera za Taifa na uanzishwaji wa mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki-GePG.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Khatibu Kazungu amemhakikishia Waziri Mpango kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa ukamilifu ili kuboresha utendaji kazi wa Wizara hiyo.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Social Plugin