Yanga SC imeendeleza rekodi yake ya kutoshinda Uwanja wa Namfua mjini Singida, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji, Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo jioni.
Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu, Yanga ikicheza bila kushinda ikitoka kufungea 1-0 na Stand United Shinyanga na kutoa sare ya 1-1 na Coastal Union Tanga, baada ya mwanzo mzuri katika mzunguko wa kwanza ikiongoza kwa tofauti ya tisa.
Kwa matokeo hayo, Yanga inajiongezea pointi moja tu na kufikisha 55 katika mechi ya 22, sasa ikiizidi point inane Azam FC, ambayo hata hivyo ina mechi mbili mkononi.
Mchezo wa leo ulikuwa mkali na timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini zilikosa maarifa ya kumalizia tu.
Mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo kwa mara nyingine leo ameendelea kucheza chini ya kiwango chake tangu amerejea kutoka kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wiki tatu zilizopita.
Nahodha Ibrahim Ajibu alianzishiwa benchi leo kabla ya kuingia kipindi cha pili, lakini naye kwa mara nyingine hakuwa na mchezo mzuri, huku kocha Mkongo, Mwinyi Zahera akimuanzisha chipukizi Gustavo Simon katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye mvua kali kwa dakika 10 za mwisho.
Mechi nyingine za leo Tanzania Prisons imeshinda 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Kagera Sugar imefungwa 1-0 na Mbeya City Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Stand United imeifunga 2-0 Ndanda FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Lipuli FC imeshinda 1-0 dhidi ya KMC Uwanja wa Samora, Iringa na JKT Tanzania imeshinda 3-1 dhidi ya Biashara United Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni .
Kikosi cha Singida United kilikuwa; Said Lubawa, Jonathan Daka, Mohammed Abdallah, Salum Kipaga, Kennedy Juma, Yussuf Kagoma, Boniface Maganga, Kenny Ally, Habibu Kiyombo/Frank Mkumbo dk83, Mathew Michael/Rajab Zahir dk71 na Athanas Mdamu/Geoffrey Mwashiuya dk64.
Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Mwinyi Mngwali, Kelvin Yondani/Andrew Vincent ‘Dante’ dk59, Abdallah Hajji ‘Ninja’, Feisal Salum/Ibrahim Ajibu dk67, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Heritier Makambo, Matheo Anthony/Pius Buswita dk59 na Gustavo Simon.
Chanzo - Binzubeiry blog