Timu ya Yanga imezinduka baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Ushindi huo wa kwanza ndani ya mechi nne za Ligi Kuu ikitoka kufungwa 1-0 na Stand United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na sare mfululizo, 1-1 na Coastal Union hapo hapo Mkwakwani na 0-0 na Singida United Uwanja wa Namfua, Singida unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 58 baada ya kucheza mechi 23.
Na hiyo inamaanisha Yanga sasa inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 10 zaidi ya Azam FC wanaofuatia katika nafasi ya pili, ingawa wana mechi mbili mkononi, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 36 za mechi 15.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Heri Sasii aliyesaidiwa na Soud Lila na Shaffid Mohammed, bao pekee la Yanga limefungwa na kiungo Mzanzibari, Feisal Salum Abdallah, maarufu kwa jina la utani Fei Toto dakika ya 26 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia krosi ya beki Gardiel Michael kutoka kushoto.
Yanga walioonekana kuathiriwa na uchovu wa kucheza mechi tatu ndani ya wiki moja mikoa miwili tofauti, leo walionekana kucheza kwa maarifa mno, muda mwingi wakiwa kwenye eneo lao na hawakutaka kutumia nguvu katika kuwania mipira dhidi ya wachezaji wa JKT Tanzania.
Hali hiyo iliwafanya waelemewe na kuzidiwa umiliki wa mpira, ingawa safu ya ulinzi ikiongozwa na kipa chipukizi Ramadhani Awam Kabwili ilitekeleza majukumu yake vizuri kwa kuokoa.
Kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alimuingiza kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ kumalizia dakika 30 za mwisho za mchezo, lakini alionekana kuathiriwa na kuwa nje muda mrefu akitumikia adhabu yake ya kufungiwa miezi 14 kwa kosa la kuvuta bangi.
Kwa mara nyingine leo, Nahodha Ibrahim Ajibu alishindwa kumaliza mechi baada ya kutolewa dakika 25 za mwisho akimpisha Deus Kaseke.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, KMC imelazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Alliance FC ya Mwanza Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam. Abdul Hillary alianza kuifungia KMC dakika ya 50, kabla ya Israel Patrick kuisawazishia Alliance dakika ya 64.
Kikosi cha JKT Tanzania kilikuwa; Patrick Muntary, Anuary Kilemile, Dickson Chota/Ally Bilal dk59, Frank Nchimbi, Mohammed Fakhi, Geeorge Mande, Hassan Matelema, Mwinyi Kazimoto, Samuel Kamuntu/Said Luyaya dk75, Ally Ahmed ‘Shiboli’/Najim Magulu dk89 na Edward Songo.
Yanga ; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa ‘Banka’ dk59, Papy Kabamba Tshishimbi, Amissi Tambwe, Pius Buswita/Kelvin Yondan dk75 na Ibrahim Ajibu/Deus Kaseke dk67.
Via>>binzubeiry
Social Plugin