YANGA YAPIGWA FAINI


Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, katika kikao chake Februari 12, 2019 ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi pamoja na malalamiko yaliyowasilishwa mbele yake na kufanya maamuzi ikiwemo kuipiga faini Yanga.

Kamati imepitia ripoti ya mechi namba 239 iliyowakutanisha wenyeji Coastal Union dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Mbali na Yanga, Coastal Union pia imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuoneshwa kadi zaidi ya tano katika mchezo huo uliofanyika Februari 3, 2019. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43(10) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa klabu.

Kamishna wa mechi hiyo Charles Mchau, na Mwamuzi Nassoro Mwinchui wamefungiwa miezi mitatu kila mmoja kutokana na taarifa zao kuwa na upungufu, na kushindwa kuumudu mchezo huo. Adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makamishna, na Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post