Yanga SC imetoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Huo ni ushindi wa kwanza kabisa kwa Yanga dhidi ya Mabo FC Uwanja wa CCM Kirumba, baada ya awali kufungwa mechi zote mbili za msimu uliopita.
Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amesema alijua leo ndiyo mwisho wa Mbao FC kuizuia Yanga kupata matokeo kwenye dimba la CCM Kirumba baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya mchezo Zahera amekiri kuwa baada ya kufungwa bao dakika za mwisho kipindi cha kwanza, aliwaambia wachezaji wake kuwa wakumbuke leo ndio siku ya mwisho ya kufungwa na Mbao FC.
''Sikujisumbua wakati wa mapumziko kuwaambia wachezaji wangu mapungufu ya Mbao FC badala yake niliwaambia kila mchezaji aseme leo ni mwisho na wakalibeba hilo wakaenda kupata matokeo'', amesema Zahera.
Kwa ujumla katika Ligi Kuu, timu hizo zimekutana mara tano na Yanga imeshinda mechi nne ikiwemo ya leo na zote tatu za Dar es Salaam, wakati Mbao wameshinda mechi mbili zilizopita za Mwanza.
Ushindi wa leo unazidi kuwafanya Yanga SC waendelee kuongoza Ligi Kuu, sasa wakifikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 25, wakifuatiwa na Azak FC yenye pointi 50 za mechi 24 na mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 42 za mechi 17.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Robert Ndaki alianza kuifungia Mbao FC kwa kichwa dakika ya 45 na ushei akimalizia krosi ya Amos Charles kutoka upande wa kushoto.
Mshambuliaji Heritier Ebenezer Makambo akaisawazishia Yanga dakika ya 50 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Papy Kabamba Tshishimbi, wote wa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao la ushindi kwa penalti dakika ya 68 baada ya beki Erick Muliro wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Kelvin Yondan kwenye boksi.
Baada ya mabao hayom timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Yanga SC walicheza kwa tahadhari zaidi kuulinda ushindi wao.
Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Metacha Mnata, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Erick Mulilo, Ally Mussa, Said Junior, Ibrahim Hashim, Pastory Athanas, Bernard Gervas/Babilas Chitembe na Ndaki Robert/Egbert Lukindo.
Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa ‘Banka’, Haruna Moshi ‘Boban’, Heritier Makambo, Amissi Tam.
Social Plugin