Kuelekea mchezo wa watani wa jadi kesho, kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ameweka wazi kuwa katika mchezo wa kwanza dhidi ya Simba, waliingia wakiwa na matatizo ikiwemo kutokuwa na maandalizi mazuri.
Zahera ameyasema hayo leo katika mkutano wake na wanahabari, ambapo amesema jambo hilo kwa sasa halipo kwani wapo vizuri na mchezo wa kesho utakuwa mzuri kushinda ule wa kwanza ambao muda mwingi walitumia kujilinda kuliko kushambulia.
''Watu waje uwanjani kwa wingi mchezo utakuwa mzuri sana maana tunaongoza ligi na tumejiandaa vizuri yale matatizo hayapo tena'', amesema Zahera.
Kwa upande mwingine Zahera amesema kitendo cha mpaka sasa timu yake kuongoza ligi kumeijengea hali ya kujiamini kwani mwanzo waliona wanaweza kumaliza hata nafasi ya 5 au 6 lakini sasa wapo kwenye nafasi nzuri.
Mchezo huo utaanza saa 10:00 jioni ambapo Yanga iliyocheza mechi 23 mpaka sasa ikiwa inaongoza ligi na pointi 58 wakati Simba ambayo ipo nafasi ya 3 ina pointi 36 katika mechi 15.
Chanzo- EATV