Shirika lisilo la Kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) la mkoani Shinyanga linalotetea haki za watoto limeunda Mabaraza ya Watoto ngazi ya vijiji katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kwa lengo la kuwajengea uwezo watoto kupaza sauti dhidi ya vitendo ya vya ukatili ambayo huwa wanafanyiwa, ikiwemo kupewa ujauzito na kuozeshwa ndoa za utotoni.
Zoezi la uundaji wa Mabaraza ya watoto limeendeshwa leo Machi 2, 2019 na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Aisha Omari kwa kushirikiana na Shirika la Agape, ambapo jumla ya mabaraza matano yameundwa katika kijiji cha Chembeli, Mwanono, Didia, Mwamalulu na Bukumbi.
Akizungumza wakati wa uundaji wa Mabaraza hayo, Meneja Mradi wa Kuzuia Mimba na Ndoa za Utotoni kutoka Shirika la AGAPE Mustapha Isabuda, amesema Mabaraza hayo ya watoto yatakuwa chachu kubwa ya kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya watoto.
Alisema watoto wanapokuwa wanakutana kwa pamoja wao wenyewe kupitia mabaraza hayo, huwa wanakuwa wawazi kuelezea changamoto za matukio ya kikatili ambayo huwa wanatendewa na baada ya hapo viongozi wao huziwasilisha kwenye mamlaka husika akiwemo mtendaji wa kijiji na hatimaye kutatuliwa.
“Tumeunda Mabaraza haya ya watoto ngazi ya vijiji katika kata ya Didia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wetu wa kupinga mimba na ndoa za utotoni, ambao unafadhiliwa na Shirika la kimataifa la FireLight Foundation kutoka nchini Marekani ambapo kwenye kata hii kuna matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto,”alisema Isabuda.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Shinyanga Aisha Omari alipongeza uundaji wa mabaraza hayo ya watoto na kutoa wito kwa watoto wayatumie vizuri ili kujikomboa na kupata haki zao za msingi, ikiwemo kutobaguliwa, kupewa elimu hasa kwa watoto wa kike na kutoozeshwa wangali watoto.
Kwa upande wao watoto hao akiwemo Nyamisi Singu ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la watoto katika kijiji cha Bukumbi alisema mabaraza hayo yatakuwa msaada mkubwa sana kwao kwani idadi kubwa ya watoto huwa wanaogopa kuelezea changamoto zao kwa watu wakubwa, na mwisho wa siku wanaambulia ujauzito ama kuozeshwa ndoa za utotoni.
Wenyeviti waliochaguliwa kuongoza wenzao katika Mabaraza ya watoto, ni Yusuf Sita (kijiji cha Mwanono), Aloyce Masele (Chembeli), Ashraf Salumu (Didia), Paschal Maganga (Mwamalulu) na Nyamisi Singu (Bukumbi).
Wengine ni Karoline Issaya ambaye amechaguliwa kuwa Makamu mwenyekiti baraza la watoto kijiji cha Mwanono ,katibu ni Ramadhani Frank, Chembeli Makamu mwenyekiti ni Milembe Maila ,katibu ni Sofia Sudi, Didia Makamu mwenyekiti ni Mwanne Emmanuel ,katibu Sundy Mayala, Mwamalulu Makamu mwenyekiti ni Scholastika Kidaha, katibu Pendo Hassani, Bukumbi Makamu mwenyekiti ni Elivida Kabuga, katibu akiwa ni Ramadhani Mrisho.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Meneja Mradi wa Kuzuia Mimba na Ndoa za utotoni kutoka Shirika la Agape la kutetea haki za watoto mkoani Shhinyanga Mustapha Isabuda ,akizungumza na watoto juu ya umuhimu wa Mabaraza ya watoto namna yatakavyoweza kuwasaidia kutokomeza matukio ya ukatili dhidi yao na kuweza kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu, pia kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Ofisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Aisha Omari akiwataka watoto kuyatumia vizuri Mabaraza ya watoto katika kupaza sauti juu ya matukio ya ukatili dhidi yao ili yapate kufanyiwa kazi kabla ya kuwaletea madhara.
Ofisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Aisha Omari, akiwasisitiza watoto kuacha kuficha matukio ya ukatili wanayofanyiwa bali wayafichue ili wawe salama na kuweza kutimiza ndoto zao.
Ofisa Maendeleo ya jamii Kata ya Didia wilaya ya Shinyanga Felista Mell, akielezea hali ya matukio ya ukatili kwenye kata hiyo ikiwemo utekelezaji wa watoto pamoja na kupewa wanafunzi kupewa mimba, ambapo kwa mwaka huu tayari wanafunzi watatu wa shule za msingi wana ujauzito na wameshaachishwa masomo, na kuwataka watoto hao wavunje ukimya watoe taarifa mapema ya matukio ya ukatili.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Jackson Majenga, akiwataka watoto hao kupitia viongozi wa mabaraza yao, kumpelekea pia taarifa za matukio ya kikatili ili ayafanyie kazi, ambapo mpaka sasa wameshamkamata mtuhumiwa mmoja wapo ambaye amempachika mimba mwanafunzi huku wengine wawili wakiendelea kutafutwa.
Watoto wakiwa kwenye mkutano wa kuunda Mabaraza yao, wakisikiliza nasaha kutoka kwa viongozi wa serikali na Shirika la Agape juu ya kuyatumia mabaraza kupaza sauti na kupata haki zao za msingi.
Watoto wakiendelea kusikiliza nasaha za viongozi kabla ya kuanza uchaguzi wa kuunda mabaraza yao ambayo yatakuwa msaada mkubwa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi yao likiwemo na suala la mimba na ndoa za utotoni na hatimaye kutimiza ndoto zao.
Watoto wakiendelea kusikiliza kwa makini namna ya kutumia Mabaraza yao kutoa taarifa za matukio ya kikatili dhidi yao, ikiwemo fursa ya kupata elimu hasa kwa watoto wa kike na kutoozeshwa ndoa za utotoni kwa tamaa ya wazazi kutaka mifugo.
Viongozi wa Baraza la watoto katika kijiji cha Chembeli ambao wamechaguliwa wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa baraza hilo Aloyce Masele katikati ni Makamu mwenyekiti Milembe Maila, akifuatiwa na katibu Sofia Sudi.
Ashraf Salum (kulia) amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la watoto katika kijiji cha Didia akiwa na makamu wake Mwanne Emmanuel.
Nyamisi Singu (wa kwanza kulia) amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la watoto katika kijiji cha Bukumbi, katikati ni Makamu wake Elivida Kabuga na wa kwanza kushoto ni Katibu Ramadhani Mrisho.
Watoto wakipewa juisi mara baada ya kumaliza kuunda Mabaraza na kuchagua viongozi wao.
Uchukuaji wa juisi ukiendelea.
Watoto wakifurahi pamoja na Ofisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya Aisha Omari, mara baada ya kumaliza kuunda Mabaraza na kuchagua viongozi ambao watakuwa wakiwaongoza katika mikutano ya kujadili changamoto ambazo huwa zinawakabili juu ya matukio ya ukatili dhidi yao ili yatatuliwe.
Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
Social Plugin