Shirika la Agape AIDS Control Programme kupitia shirika la Firelight Foundation la nchini Marekani limetoa msaada wa mbuzi na kondoo 40 kwa kaya 10 zenye uhitaji katika kata ya Didia Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kuwasaidia watoto wa kike wanaosoma kutoka familia hizo wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuepuka mimba na ndoa za utotoni.
Msaada huo wa mifugo hao wenye thamani ya shilingi milioni tatu umetolewa leo Jumamosi Machi 30,2019 katika viwanja vya shule ya msingi Didia ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mifugo hao (mbuzi19 na kondoo 21), Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola alisema ni kwa ajili ya kaya 10 zenye uhitaji lengo likiwa ni kuwafikia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Msaada huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wetu wa Kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa ufadhili wa shirika la Firelight Foundation la nchini Marekani, tunaamini kuwa tukiwezesha wazazi wao kwa kuwapa mifugo basi tutakuwa tumesaidia watoto wa kaya hizo wanaosoma kuwa katika mazingira salama ili kuondokana na vitendo vya kuolewa au kupata mimba vinavyochangiwa na umaskini”,alieleza Myola.
“Kaya hizi ambazo kila moja leo zitapata mbuzi na kondoo wanne hazitokani na Mpango wa kunusuru kaya Maskini (TASAF),bali Agape kwa kushirikiana na baraza la maendeleo la vijiji lilibaini kaya hizi 10 ambapo tumechukua kaya mbili kila kijiji kutoka vijiji vya Mwamalulu,Mwanono,Bukumbi,Didia na Chembeli na pindi mifugo hao watakapozaana kaya zingine zitapewa mifugo waliozaliwa”,alifafanua Myola.
Myola alisema shirika lake linaunga mkono serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kuwajengea uwezo kiuchumi wananchi na kukabiliana na ndoa na mimba za utotoni.
Kwa upande wake,Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi alilipongeza shirika la Agape kwa kuendelea kushirikiana na serikali kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Aidha aliziasa familia/kaya zilizopata msaada huo kutumia mifugo hao kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujiinua kiuchumi huku akiwataka watendaji na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanasimamia mifugo hiyo ili iendelee kunufaisha familia nyingi zaidi.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akizungumza wakati wa kukabidhi mbuzi na kondoo 40 kwa kaya 10 zenye uhitaji katika kata ya Didia Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Kulia kwake ni Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi (aliyevaa shati la kitenge) akifuatiwa na Diwani wa kata ya Didia,Richard Masele (aliyebeba kondoo) pamoja na wawakilishi wa kaya hizo.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akitoa mwongozo wa kugawa kondoo/mbuzi wanne kwa kila kaya.
Sehemu ya kondoo na mbuzi waliotolewa na shirika la Agape kwa familia 10 zenye uhitaji katika kata ya Didia ambapo kila kaya imepata mbuzi/kondoo wanne.
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi (mwenye shati la kitenge) akipokea mbuzi/kondoo kutoka shirika la Agape.
Zoezi la kukabidhi mbuzi likiendelea.
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi akiwasisitiza wananchi waliopata msaada wa mbuzi na kondoo kutumia mifugo hao kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akizungumza baada ya kukabidhi kondoo na mbuzi kwa kaya 10 zenye uhitaji zilizopo katika kaya ya Didia.
Diwani wa kata ya Didia,Richard Masele akilipongeza shirika la Agape kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi wa Didia kwani limekuwa likitoa misaada mbalimbali ili kuhakikisha mimba na ndoa za utotoni zinatokomezwa katika kata hiyo.
Bibi Njile Kulwa akitoa neno la shukrani kwa shirika la Agape kwa kuwapatia msaada wa mbuzi wawili na kondoo wawili.
Bibi Njile Kulwa akiwa amesimama wakati mbuzi na kondoo wake wakifungwa kamba tayari kwa kuondoka nao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mbuzi 19 na kondoo 21 kwa ajili ya kaya 10 zenye uhitaji kutoka kata ya Didia (kaya mbili kila kijiji kwenye vijiji vitano vya kata hiyo).
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi akizungumza wakati wa kupokea mbuzi 19 na kondoo 21 waliotolewa na shirika la Agape kwa ajili ya kaya 10 zenye uhitaji katika kata ya Didia.
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi akikabidhi kanga,kitenge na shuka nyeusi kwa Bi. Salma Machiya ikiwa ni zawadi kutoka shirika la Agape kwa wema aliouonesha kwa kutunza mbuzi na kondoo 40 kwa muda wa wiki moja wakisubiri kugawiwa kwa kaya 10 leo.
Binti wa Bi. Salma Machiya, naye akipokea zawadi ya madaftari na kalamu kwa ajili ya masomo yake katika shule ya Sekondari Itwangi.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog