Takriban watu 50 waliokuwa wakisafiri na basi Abood wamenusika kifo na kujeruhiwa baada ya gari kuacha njia na kukigonga kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo maeneo ya Kimara Corner wilayani Ubungo.
Mkuu wa operesheni wa kikosi cha usalama barabarani (Trafiki), Abdi Isango amesema ajali hiyo ilitokea leo Alhamis Machi 7,2019 saa 12: 30 asubuhi na chanzo chake ni mwendokasi wa dereva wa basi la Abood.
"Basi la Abood ambalo ni Marcopollo lilikuwa katika mwendokasi likimbizana na basi lingine. Lilipofika maeneo hayo lilitaka kuovataki basi la mbele yake lakini kutokana kutokuwa makini wa kuacha nafasi alijikuta akiingia upande wa barabara ya mwendokasi na kuharibu miundombinu yake.
"Baada ya kuona nafasi ndogo kati ya basi jingine na ili asiligonge aliamua kuparamia barabara hiyo. Ameharibu nguzo za barabara hiyo na kituo pia gari lake kuharibika," amesema Isango.
Isango alisema hakuna madhara kwa abiria wa gari hilo na waliokuwamo katika kituo hicho na gari hilo limepelekwa Kituo cha Polisi Mbezi huku dereva wake akishikiliwa kwa mahojiano.
Na Bakari Kiango, Mwananchi
Social Plugin