Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema kuwa hatotumia tena salamu za kidini katika mikutano ya hadhara ili kutokiletea chama chake matatizo ya kisheria.
Ameyasema hayo mara baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukionya na kukitaka kujieleza Chama Cha ACT- Wazalendo baada ya kutumia salamu za kidini kinyume na sheria ya vyama vya siasa nchini.
Amesema kuwa hatotumia tena salamu hizo ambazo zitapelekea chama cha Mapinduzi (CCM) kuonekana kwamba kinabagua wasio na dini.
“Kuanzia leo nikienda kwenye mikutano ya hadhara situmii salaam kama “Assalaam Alykum” or “Bwana Yesu Asifiwe” nisije nikakiletea matatizo chama chetu CCM nakuonekana kinabagua wasiokua na dini. “tafakuri yangu tahadhari kabla ya mauti”.ameandika Bashe kwenye ukurasa wake wa kijamii.
Aidha, tafakuri hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransic Mutungi kutishia kukifuta Chama Cha ACT- Wazalendo kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwamo kuchoma moto bendera ya Chama cha Wananchi (CUF) huku wakitumia maneno ya kidini.
Hata hivyo, sehemu ya taarifa ya msajili wa siasa ilisema kwamba, “vile vile katika mitandao ya kijamii imeonekana video watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislamu (Takbir), kitendo hiki pia ni kukiuka kifungu cha (9) (1) (c) cha Sheria ya Vyama vya Siasa inayokataza kuwa na ubaguzi wa kidini kwa wanachama wake na kifungu cha (9) (2) (a), kinachokataza katiba, sera au vitendo vya chama cha siasa kuhamasisha au kueneza dini fulani”
Social Plugin