Mtandao wa kijamii wa Facebook kwa sasa unakumbwa na hali mbaya zaidi ya mawasiliano kuwahi kutokea katika historia yake kwani huduma nyingi hazipatikani kote ulimwenguni.
"Tunafahamu kuwa baadhi ya watu hawawezi kufikia app zinazohusiana na Facebook ," ilisema taarifa iliyotolewa na Facebook.
Haijabainika wazi ni nini kinachosababisha shida hiyo.
"Tunafanya kila juhudi kushughulikia tatizo lililopo haraka iwezekanavyo."
Kando na Facebook yenyewe, huduma za Messenger na Instagram zimetatizwa.
Mara ya mwisho Facebook ilijipata katika hali hiyo ilikuwa mwaka 2008 wakati mtandao huo ulikuwa na watumiaji milioni 150 -ikilinganishwa na sasa ambapo watumiaji karibu wanakadiriwa kuwa karibu bilioni 2.3 kwa mwezi.
Kampuni ya Facebook imejibu uvumi unaoendelea mitandaoni kuwa huenda mtandao huo maarufu duniani umedukuliwa.
Inasema hali hiyo haijatokana na shambulio lolote la kimtandao
Tatizo ni kubwa kiasi gani?
Inakadiriwa kuwa tatizo hilo lilianza kukumba mtandao huo siku ya Jumatano.
Japo huduma ya Facebook ilionekana kuwa sawa watumiaji wake waliripoti kuwa na hawawezi kutuma ujumbe.
Watumiaji wa Instagram hawawezi kufikia ujumbe mpya huku wale wanaotumia huduma ya Facebook Messenger kupitia kompyuta pia wakikabiliwa na changamoto sawia na hiyo.
Hata hivyo watumiaji wa mtandao huo kupitia app ya simu waliweza kutuma baadhi ya ujumbe japo nao pia walielezea kupata changamoto ya kutuma picha.
Mtandao wa WhatsApp, pia uliathiriwa na changamoto hizo.
Hali hiyo imeathiri kampuni zinazotumia Facebook kuendesha biashara zao kwasababu walishindwa kabisa kuwasiliana.
Mwana mitindo Rebecca Brooker ambaye anatumia mtandao huo kufanya kazi yake mjini Buenos Aires ameiambia BBC kuwa hali hiyo imeathiri pakubwa biashara yake.
"Facebook kwa matumizi ya kibinafsi ni sawa lakini kwa kampuni kubwa zinazoendesha huduma zao kupitia mtandao huo unatarajia hii inamaanisha nini kwao?" alisema.
Nchini Uingereza mshauri n a mtaalamu wa magonjwa ya watoto aliiambia BBC kuwa wafanyikazi wenzake walisikitika na kukatizwa kwa huduma hizo kwa sababu walikuwa na hafla ya kumuaga muuguzi mmoja ambaye amehudumu kwa miaka 20.
"Ilikuwa siku ya kazi na washauri wengi hawakuweza kufika lakini walitegemea kutumia whatsApp kujumuika pamoja," alisema Dr Nikhil Ganjoo.
"Kwa hivyo nililazimika kuwakilisha lakini sikuweza hata kuwatumia picha za matukio katika hafla hiyo."
Tatizo hilo linatokea wakati wabunge nchini Marekani wanatafakari uwezekano wa kuvunjilia mbali makampuni makubwa ya teknolojia - si tu Facebook.
Chanzo - BBC
Social Plugin