Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake watano iko katika mchakato wa kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
“Mheshimiwa Hakimu, Jamhuri tupo kwenye mchakato wa kuwasilisha taarifa za kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,” alidai Wakili wa Serikali, Estazia Wilson.
Wakili Estazia alidai bado hawajawasilisha taarifa katika mahakama hiyo ili waweze kupewa vijalada na kuwezesha kusomwa kwa maelezo ya mashahidi.
Hakimu Ally aliutaka upande wa mashtaka kuharakisha mchakato huo ili tarehe ijayo waje na maelezo tofauti.
Kutokana na hali hiyo, Estazia aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo ambapo Mahakama ilipanga Aprilii 4 mwaka huu.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Meneja Biashara wa NIDA, Aveln Momburi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Katika kesi hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 100 yakiwamo 24 ya kutakatisha fedha, kughushi 23, kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri 43 na matano ya kuisababishia hasara NIDA.
Pia, yapo mashtaka mawili ya kula njama ya kulaghai, mawili ya matumizi mabaya ya madaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka lipo moja ambalo linawakabili Maimu na Sabina.
Social Plugin