Rashid Mustapha akivaa nguo baada ya kumchoma kisu mkononi Daniel Mtambala Gudugudu - Picha na William Bundala
Kijana aliyejulikana kwa jina la Daniel Mtambala Gudugudu (30 mkazi wa Nyihogo Mjini Kahama ameuawa kwa kuchomwa na kisu kwenye mkono wa kushoto na Rashid Mustapha (48) mkazi wa Nyihogo wilaya ya Kahama.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao tukio hilo limetokea Machi 9,2019 majira ya saa 12 jioni eneo la Nyihogo Transfoma, kata ya Nyihogo Mjini Kahama.
“Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na kudaiana viatu raba nyeusi, mbinu iliyotumika ni kumchoma kisu mkono wa kushoto na kusababisha damu nyingi kutoka”,ameeleza Kamanda Abwao.
"Daniel alikuwa anadai arudishiwe viatu vyake,na katika ugomvi huo wakaanza kushambuliana ndipo aliyenyang'anywa viatu,akachomwa kisu na kusababisha kifo chake",ameeleza Kamanda Abwao.
Amesema tayari mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema watu hao walikuwa wamelewa na kwamba aliyeua mwenzake alikuwa ana mdai pesa zilizotokana na kuuziana nyama,katika kudaiana huko ndipo mtuhumiwa akachukua viatu vya marehemu, marehemu akahamaki baada ya viatu vyake kuchukuliwa ugomvi ukaanza akidai arudishiwe viatu vyake ndipo akaambulia kuchomwa kisu.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin