Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWALIMU ALIYEPIGA MWANAFUNZI HADI KUMUUA BUKOBA AHUKUMIWA KUNYONGWA



Mwalimu Respicius Mtazangira amehukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha kifo cha mwanafunzi wa shule ya msingi Kibeta Sperius Eradius.

Mtazangira amehukumiwa leo tarehe 6 Machi 2019 huku Mahakama hiyo ikimuachia huru aliyekuwa mshtakiwa mwenza katika kesi ya mauaji ya kukusudia, Mwalimu Herieth Gerald.

Kesi hiyo ilifunguliwa mwishoni mwa mwaka jana na kusikilizwa na Jaji Lameck Mlacha ambaye leo alisoma hukumu ya kesi hiyo.

Walimu hao walishitakiwa kwa kumuua kwa kukusudia Sperius Eradius aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo mwishoni mwa mwaka 2018.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi tisa katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa mwezi mmoja na Jaji Lameck Mlacha, ilianza Februari 6, 2019.

Inadaiwa walimu hao walitenda kosa la kumuadhibu kwa kipigo mwanafunzi Sperius Eradius kwa madai kuwa aliiba mkoba wa mwalimu ukiwa na fedha.

Tukio hilo lilitokea tarehe 27 Agosti 2018, ambapo marehemu Sperius aliyekuwa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta (14) alipigwa na mwalimu Mtazangira akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu Herieth.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com