Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo Ijumaa Machi Mosi, 2019 ametangaza uamuzi wa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa amerejea katika chama chake cha zamani shughuli iliyofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Uamuzi wa Lowassa kutangaza kurejea CCM ameuchukua ikiwa imepita miaka mitatu tangu alipotangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema Julai 28, 2015 baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kuwania urais mwaka 2015.
Akizungumza leo katika Ofisi za ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam,Lowassa hakuwa na maneno mengi ya kueleza zaidi ya kuwaambia Watanzania kuwa ameamua kurudi nyumbani (CCM).
"Nimetafakari na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa huko,"amesema Lowassa huku mamia ya wananchi wakiwamo wanachama na wapenzi wa CCM walikuwa wanamshangilia.
Shughuli ya kumpokea Lowassa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vya Ukawa vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi imehudhuriwa na wanachama mbalimbali na wananchi wachache waliokuwapo.
Akizungumza kwa kifupi, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema, “Ametangaza kurudi nyumbani na tuko tayari kumpokea.”
SOMA ZAIDI HAPA
Social Plugin