Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : MAOFISA USTAWI WA JAMII SHINYANGA WATINGA GEREZANI KUSHEREHEKEA SIKU YA USTAWI WA JAMII



Maofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha Siku ya Ustawi wa Jamii kwa kutembelea wafungwa wanawake katika gereza la Shinyanga,kutoa chakula kwa kaya maskini na kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto kwa wanafunzi.



Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mkoani leo Machi 21,2019 ,Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa, Lidya Kwezigabo, alisema wameamua kutembelea wafungwa wanawake kwenye gereza la Mjini Shinyanga ambao wamefungwa na watoto wao, ili kutoa elimu ya ulinzi wa mtoto na kuweza kupata haki zao za msingi.

Alisema mbali na kutembelea wafungwa hao, pia wameona ni vyema kwenda kutoa elimu ya ukatili na kujitambua kwa wanafunzi mashuleni kwani wanafunzi ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo hivyo, lengo likiwa ni kutokomeza matukio hayo ndani ya jamii.

“Sisi Maofisa Ustawi wa Jamii mkoa Shinyanga kwa pamoja tumeamua kuadhimisha siku yetu hii kwa kutoa elimu zaidi juu ya kutomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili waweze kupata haki zao za msingi ikiwamo kutimiza malengo yao ya kielimu,”alisema Kwezigabo.

“Pamoja na kutoa elimu ya ukatili pia tumetoa msaada wa sabuni za kufulia, kuogea na dawa za mswaki kwa wanawake ambao wamefungwa kwenye Magereza ya Shinyanga pamoja na msaada wa chakula kwenye kaya maskini iliyopo kata ya Mwasele katika Manispaa ya Shinyanga,”aliongeza.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Elizabeth Mweyo aliwataka wanafunzi hao pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ama mwenzao, wawe wanatoa taarifa kwa walimu au viongozi wa Serikali ili waweze kusaidiwa na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

Pia aliwataka kuacha kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi wakiwa bado wanafunzi na kutopenda vitu vya dezo ikiwamo Lifti, vitu ambavyo vimekuwa vikiwaingiza kwenye vishawishi na kujikuta wakiambulia kupewa ujauzito na kuachishwa masomo yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Sekondari Chamaguha ambayo ilitembelewa na Maofisa  Ustawi wa Jamii Abdalla Lidyati, alipongeza utolewaji wa elimu hiyo ya ukatili na kujitambua kwa wanafunzi hali ambayo itasaidia kuondokana na mimba mashuleni.

Maadhimisho  ya siku ya Ustawi wa Jamii kitaifa yamefanyika leo Machi 21,3,2019 Jijini Arusha.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Shinyanga, Lidya Kwezigabo akizungumza kabla ya kuanza kugawa msaada wa sabuni za kufulia na kuogea pamoja na dawa za meno kwa ajili ya matumizi ya wafungwa wanawake ambao wamefungwa na watoto wao katika gereza la Shinyanga. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mkuu wa Gereza la Shinyanga Paulo sabuni Kamole (kulia) akipokea msaada wa sabuni za kufulia na kuogea pamoja na dawa za meno kutoka kwa Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Shinyanga Lidya Kwezigabo.

Mkuu wa Gereza la Shinyanga Paulo Sabuni Kamole, akishukuru msaada huo kutoka kwa Maofisa Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuwatatulia changamoto ndogo ndogo wafungwa wanawake pamoja na kuwapatia elimu ya ulinzi wa mtoto.

Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Shinyanga Lidya Kwezigabo akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Chamaguha na kuwataka wapinge masuala ya ukatili ndani ya jamii kwa kuanza na wao wenyewe.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Chamaguha Shinyanga mjini wakisikiliza kwa makini elimu ya makuzi na kupinga masuala ya ukatili ambayo yamekuwa yakizima ndoto zao.

Wanafunzi wakiendelea kusikiliza elimu ya kupinga ukatili.

Ofisa ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Elizabeth Mweyo, akiwataka wanafunzi hao hasa wa kike waache kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi wakiwa katika umri mdogo na kuacha tamaa ya kupenda chips na Lift, ili wapate kutimiza ndoto zao.

Ofisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Agnes Cinethon akiwataka wanafunzi hao hasa wa kike pale wanapobakwa wawahi kwenye vituo vya afya ili waweze kupatiwa matibabu ya haraka na kuwazuia kutopatwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa.

Ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga Sophia Kang'ombe ambaye huwa ana hudumia Kambi ya wazee Kolandoto akiwataka wanafunzi hao kupenda Babu na Bibi zao wakiwamo na wazazi ili kujenga mahusiano mazuri ambayo yatawasaidia kuwa wanatatuliwa shida zao, ikiwamo na kutoa taarifa za watu kutaka kuwafanyia ukatili na kuweza kutatuliwa.

Wanafunzi wakiendelea na upewaji wa elimu ya makuzi na ukatili.

Mwanafunzi Naomi Geogre akiuliza swali namna kesi za ukatili zitakavyoshughulikiwa pale watakapokuwa wakitoa taarifa za matukio hayo.

Mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Sekondari Chamaguha Abdalla Lidyati, akielezea kufurahishwa na ujio wa mofisa ustawi kwenye shule hiyo na kutoa elimu ya makuzi na ukatili, hali ambayo itasaidia kusiwepo na mimba shuleni hapo.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ushirika nao wakisikiliza elimu ya ukatili na kutakiwa wawe wanatoa taarifa mapema pale wanapoona kutaka kufanyiwa vitendo hivyo, ili vipate kushughulikiwa kabla ya kuwaletea madhara.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Elizabeth Mweyo akitoa elimu ya kupinga ukatili kwa wanafunzi wa shule ya msingi Ushirika. 

Zoezi la kutoa chakula likiendelea katika moja ya kaya katika kata ya Mwasele katika manispaa ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com