Madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na saratani nchini, wamesema, ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, matiti na Ukimwi ni magonjwa matatu hatari zaidi kwa wanawake nchini, kwa kuwa yanaua taratibu na kudhoofisha nguvukazi ya taifa kwa kasi.
Wamesema kwa nyakati tofauti kuwa, magonjwa hayo yanachangia vifo na kudhoofisha nguvu kazi ya taifa hasa kwa wanawake na yanachangiwa na kutokuwa na uelewa sahihi wa vyanzo vyake, imani za kishirikina, malezi mabaya ya familia na mila potofu.
Kwa mujibu wa madaktari hao, athari za magonjwa haya hazionekani kwa idadi kubwa ya vifo vya mara moja, lakini madhara yake ni makubwa kwa kuwa hudhoofisha mwili na kuua taratibu.
Aidha, wameshauri serikali iendelee kuweka nguvu kubwa kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo kama inavyofanya sasa, hasa katika eneo la chanjo kwa saratani ya mlango wa kizazi na uchunguzi wa awali kwa saratani hiyo na ile ya matiti.
Wakati wataalamu hao wakieleza hayo, serikali inasema inatambua kuwa magonjwa hayo ni hatari kwa jamii hasa kwa wanawake na ili kuyakabili, inahimiza watu kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kama wameathiriwa na hivyo, kupata tiba na ushauri mapema.
Serikali pia inawataka wazazi kuhakikisha watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14, wanachunguzwa na kupata chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Vicent Tarimo, anasema saratani ya mlango wa kizazi, ya matiti na Ukimwi, ni magonjwa hatari kwa wanawake.
Saratani ya mlango wa kizazi Dk Tarimo, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika MNH, anasema mwaka 2017 na 2018, asilimia 30 mpaka 40 ya wagonjwa wanawake waliolazwa wodini, walikuwa na saratani ya mlango wa kizazi na hali hiyo ipo mpaka sasa. Dk Tarimo anasema huu ni ugonjwa wa kwanza hatarishi kwa afya ya wanawake nchini.
Anasema kwa sasa hali inatisha zaidi kwani hata wasichana wadogo wenye umri wa miaka 20 na 21 wana maambukizi yasaratani hii.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mwaka jana kati ya wagonjwa wanawake 2,519 waliolazwa katika wodi mbili hospitalini hapo, 922 walikuwa na saratani ya mlango wa kizazi na 75 kati yao walifariki.
“Kiumri wanaoathirika zaidi, inawezekana ni kwa kuchelewa uchunguzi na tiba, ni kuanzia miaka 30 hadi 60, hawa ndio wengi, ingawa na wenye umri mdogo zaidi wapo,” anasema Dk Tarimo.
Anasema njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni kutia mkazo katika chanjo, kazi ambayo tayari serikali inaifanya vizuri na kufanyika kwa uchunguzi wa awali. Alisema njia hizo zinapunguza tatizo la saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 98.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Julius Mwaiselage, pia anasema magonjwa hayo ni tishio kwa wanawake. Anasema mwaka jana walipokea wanawake 2,196 na waliokutwa na tatizo ni 1,287 huku vifo vikiwa 78.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 zinaonesha kuwa, katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kuwa na wanawake wengi wenye saratani ya mlango wa kizazi.
Hata hivyo, huenda kiwango hiki kikubwa kinatokana na mwitikio chanya wa wanawake wengi kupima na kujua kama wana maambukizi ikilinganishwa na nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa WHO, mwaka 2012 wanawake 51 waligundulika kuwa na saratani hiyo kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000.
Satarani ya mlango wa kizazi husababishwa na maambukizi ya virusi viitwavyo Human Papilloma Virus (HPV) na hutokana na ngono zembe.
Saratani ya matiti Kuhusu saratani ya matiti, hospitali ya Ocean Road, mwaka jana katika eneo la uchunguzi wa saratani hiyo, ilipokea wagonjwa wanawake 971 na waliokutwa na saratani ya matiti walikuwa 432 huku vifo vikiwa 62.
Dk Mwaiselage anasema kwa sasa tatizo hilo ni kubwa na linapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa hasa kwa wanawake wote nchini kuhakikisha wanafanyiwa uchunguzi mapema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Ibrahim Mkoma ambaye idara yake ndiyo inayoshughulika na saratani ya matiti hospitalini hapo, anasema wagonjwa wengi wanafika hospitalini wakiwa wamechelewa.
Dk Mkoma anasema wengi wanafika hospitalini wakiwa katika hatua ya tatu na nne ambazo ni hatua za mwisho zinazochangia mgonjwa kutopona.
Kwa mujibu wa Dk Mkoma, asilimia 10 hadi 20ya wagonjwa wanawake wanaolazwa katika wodi za upasuaji katika hospitali hiyo wana saratani ya matiti.
Ukimwi Aidha, kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko anasema kundi la vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 25, linashambuliwa zaidi na kwamba asilimia 80 ya wenye maambukizi ni wasichana na wavulana ni asilimia 20.
Wakati akizungumza katika Wiki ya Maonesho ya Huduma kuelekea Siku ya Ukimwi Duniani mwaka 2019, Dk Maboko alisema hali hiyo inamaanisha kuwa, katika kila vijana 10 wenye VVU, wanane ni wasichana na wawili ni wavulana.
Anasema tafiti wanazofanya mara kwa mara zinaonesha kuwa watoto wa kike wa umri wa miaka 10 hadi 12 wengi wao wakiwa darasa la tano na la saba, wanaanza kujamiiana tena na wanaume wengi na hii ni hatari kubwa kwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi (VVU) na saratani ya shingo ya kizazi. Imani potofu; Dk Tarimo anasema katika jamii nyingi, zipo fikra na imani za ushirikina (kurogwa) zinazochangia kwa kiasi kikubwa watu kuchelewa uchunguzi na wanapogundulika na kupangiwa tiba, kwa kuwa wengi wanadhani wamerogwa, hivyo hawafuatilii matibabu.
Anasema pia kuwa, malezi mabaya ya kuiga utamaduni wa nje kwa kuacha watoto waanze ngono mapema huku jamii ikiona kuwa ni usasa, yanachangia ukubwa wa tatizo. Hoja hiyo inaelezwa pia na Dk Maboko anayekiri kuwa, tafiti za Tacaids zinaonesha kuwa, watoto wengi wa kike wanaanza ngono; tena zembe wakiwa katika umri mdogo.
Serikali inavyochukua hatua Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile, anasema katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni kuwa, serikali inatambua hatari na ukubwa wa magonjwa hayo kwa jamii hasa wanawake na imechukua hatua kadhaa. Dk Ndugulile anasema hatua hizo zinaleta matokeo chanya, lakini bado jamii haijaelimika ipasavyo kuhusu magonjwa hayo na hivyo, baadhi ya watu kubaki katika imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa Dk Ndugulile, hali hiyo huchangia kufika hospitalini wakiwa katika hatua mbaya. Anasema jamii inapaswa kutambua kuwa uchunguzi wa awali unafanyika bila malipo katika vituo vyote vya afya vya serikali nchini na hivyo, jamii itumie fursa hiyo kikamilifu kujua hali za afya badala ya kusubiri dalili.
“Unaposubiri dalili ukiona zimeanza kutokea ujue upo katika hatari zaidi ya kusababisha usipone, serikali imejitahidi kuweka nguvu kubwa katika uchunguzi wa awali na chanjo inayoendelea kote nchini,” anasema.
Anasisitiza: “Nawaomba wazazi na walezi wenye mabinti na wanawake wote kwa jumla; wajitokeze maana huduma hizi ni bure; hazilipiwi.” Aprili 2018, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alizindua chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi iliyolenga kuwafikia takribani wasichana 600,000 wenye umri wa miaka 14.
Awamu ya pili mwaka huu ni kwa watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka tisa. Dk Ndugulile anasema kati ya wasichana 598,458 waliolengwa kufikiwa mwaka jana katika awamu ya kwanza ya chanjo iliyoisha Desemba, wamefikiwa 380,776 sawa na asilimia 64 ya lengo.
Anasema serikali haijaridhika kwa mwitikio huo na imewataka wazazi, walezi na jamii kuhamasisha zaidi umuhimu wa chanjo hiyo ili kuwakinga watoto wa kike wasipate madhara kwani ndio kizazi kinachotegemewa na Taifa.
Anasema awamu ya pili ilianza Januari mwaka huu hadi Juni na inawalenga watoto wa kike 380,776 wenye umri wa miaka 14 waliofikiwa na chanjo ya awamu ya kwanza mwaka jana. Tayari watoto 126,769 wamefikiwa mpaka sasa.
Kuanzia Juni mwaka huu watoto wa kike kuanzia miaka tisa, watapatiwa chanjo hiyo. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, nyakati mbalimbali amekuwa akiwahamasisha wazazi na jamii kuhakikisha watoto wa kike wenye umri wa miaka tisa hadi 14 wanapata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na kupuuza uzushi kwamba, zina madhara kwa kizazi kwani zimethibitishwa ubora kimataifa.
Aidha, Ummy amekuwa akihamasisha wanawake kujitokeza kuchunguzwa saratani ya matiti hasa kupitia kampeni za uchunguzi zinazoendeshwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) na kupima VVU hasa kwa wajawazito ili kumlinda kupata maambukizi mtoto aliye tumboni na kupata kizazi huru dhidi ya maradhi hayo.
Juhudi hizi za serikali, taasisi binafsi na mashirika ya kigeni zikiungwa mkono na jamii, hakika magonjwa hayo tishio yatakwisha na itabaki historia nchini. Pamoja tunaweza.