Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro.
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi katika maeneo ya Murungushi Igogo jijini Mwanza wakati wakijaribu kurushiana risasi na askari polisi waliokuwa doria.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Jumanne Muliro, amesema tukio hilo lilitokea eneo hilo la Igogo jirani na ghala la kiwanda cha Avant linalotumika kuhifadhi bidhaa za vipuli vya magari na vifaa vya ujenzi, huku majambazi wengine wakifanikiwa kukimbia baada ya kukaidi amri ya kujisalimisha.
Muliro ameongeza kuwa majambazi hao waliouawa walikuwa na silaha aina ya 'Shortgun' iliyokuwa na risasi 4, mapanga matatu, nondo moja, mkasi mkubwa wa kuvunjia milango na makufuli na pia funguo nyingi zinazotumika kufungulia milango, makufuli na droo za ofisi na maghala.
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, majambazi hao waliofariki wana umri kati ya miaka 30 hadi 35 na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa uchunguzi na utambuzi zaidi.
Pia ameeleza kuwa watuhumiwa wengine wa ujambazi waliotoroka eneo la tukio wanasakwa kwa udi na uvumba ili watiwe nguvuni na jeshi la polisi.
Social Plugin