Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma.
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limewaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamejipanga kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.
Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa Wilaya ya Kimbondo,Louis Bura ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo amesema jana usiku majira ya saa tatu Askari polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi, kuwa kuna majambazi wanataka kuvamia baadhi ya nyumba ndipo walipofika eneo la tukio na kuanza kurushiana risasi na majambazi hao.
Katika tukio hilo askari mmoja aliyefahamika kwa jina la James Mwita (37) na mama mmoja Sophia Dickson (60) walijeruhiwa na sasa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Kibondo.
Bura amesema askari huyo alipatiwa matibabu ya awali na sasa hali yake sio mbaya na amepatiwa rufaa kwa ajili ya kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kwa kuwa amejeruhika sana mguuni.
Amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama pia Jeshi la polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwa ni kazi ngumu na kwamba wananchi wataendelea kutoa ushirikiano kwa kuwa polisi wako kazini.
Ametoa rai kwa wote wanaojihusisha na matukio ya ujambazi kuacha mara moja kwa kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na matukio hayo.
Aidha amewataka wananchi kuacha kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo baadhi wanawakamata wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na kudai sio majambazi.
"Niwaambie tu wananchi hatutavumilia kuona majambazi wanaendelea kututesa Kibondo tumechoka, na kuanzia sasa niwaombe wananchi wale wanaoshirikiana na raia wa Burundi kuvamia watu muache maana jambazi hawezi kuja bila kupewa taarifa na watu ambao wanafahamu ni nani ana pesa, niseme tu kwa sasa tumejipanga tumechoka haya mambo hatuta wavumilia", alisema Bura.
Aidha amewataka wananchi kuacha kutoka nje pindi wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya usalama wao kwa kuwa ni hatari sana kufuata milio hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Kibondo Sebasitiani Pima amesema walipokea watu watatu wakiwa wamefariki naa majeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kibondo na mmoja wamemsafirisha kuelekea Kigoma kwa ajili ya matibabu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibondo Khamisi Tahilo ameipongeza serikali na polisi kwa kazi wanayoifanya na kwamba wananchi wamefurahi sana kwa kuwa wameshuhudia wenyewe kwa macho yao jambazi mmoja ambaye wamekuta amefia katika mfereji wa maji wa soko la Mjini na wametoa kiasi cha shilingi laki moja kuwapa pole askari hao.
Amesema matendo yaliyokuwa yakifanya na majambazi hao Wilayani humo yamewachosha na sasa wanafuraha sana kwa kuwa Serikali imeimarisha usalama na ikitokea tatizo lolote wanawakamata.
Kwa upande wake mmiliki wa nyumba ambayo majambazi walikuwa wamepanga kuvamia Hamis Salumu amesema alipigiwa simu na kuambiwa kwamba nyumbani kwake kuna watu wanapiga risasi ndipo alipokwenda polisi na kukuta tayari polisi walishakwenda nyumbani kwake.
Amesema hakuna aliyejeruhiwa wala kilichoibiwa nyumbani kwake na ametoa pongezi kwa jeshi la polisi kwa ushirikiano wanaouonyesha na kuwataka wengine wanaojihusisha na shughuli za ujambazi kuacha mara moja kwani mwisho wao ni mbaya.
Social Plugin